HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 09, 2020

VETA YATAKIWA KUWAFUATILIA WANAFUNZI WALIOBUNI BIDHAA MBALIMBALI

MWENYEKITI  wa bodi ya Elimu na Mafunzo ya ufundi Stadi, Peter Maduki, akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) lililopo katika maonesho ya 44 ya biashara  ya kimataifa ‘sabasaba’  yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Na Tatu Mohamed

MWENYEKITI  wa bodi ya Elimu na Mafunzo ya ufundi Stadi, Peter Maduki, ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya ufundi Stadi (VETA) kuwafuatilia na kuwaunganisha wanafunzi waliotengeneza na kubuni bidhaa mbalimbali kutoka Chuo hicho.

Pia ametoa wito kwa waajiri kutumia wanafunzi wanaotoka katika vyuo hivyo kuwaajiri kwani wanakuwa mahiri katika kazi zao na kushiriki kwenye uzalishaji moja kwa moja.

Maduki ameyasema hayo, leo Julai 9, 2020 wakati alipotembela banda la VETA katika maonesho ya 44 ya biashara  ya kimataifa ‘sabasaba’  yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Amesema vijana wamekuwa wakibuni wa kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora na imara na zinazouzika kwenye soko la nchi.

“Niwatake uongozi wa VETA kuwaunganisha wabunifu mfano waliotengeneza pikipiki  na viwanda ambavyo vinazalisha pikipiki hapa nchini,” amesema.

Ameongeza kuwa, wazalishaji wa VETA wanazingatia ubora huku akibainisha kuwa wapo wenye mtazamo wa kudhani vitu vya nje ya nchi ndivyo vyenye ubora.

“Vitu vinavyozalishwa VETA nimeviona vinaubora kuliko hata tunavyovifikiria kutoka nje, ubora huu unapatikana kutokana na malighafi zinazopatikana Tanzania,” amesema.

Ameeleza kuwa,  kupitia maonesho hayo ameweza kuona bunifu mbalimbali zinazofanywa na vijana waliopo vyuoni na hata waliohitimu masomo yao.

“Mafunzo haya wanayoyapata na kuyatumia yanaweza kusaidia kuchangia kuanzisha viwanda na kuviimarisha, kukuza ajira kwa vijana wanaomaliza katika vyuo mbalimbali,” amesema.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo si tu  yanatoa ajira bali huwasaidia hata wale walio katika maeneo yao ya kazi kama kwenye kilimo na ufugaji ambapo wanaweza kujifunza kwa muda mfupi na kuongeza tija katika maeneo yao.

“Haya ni mambo makubwa , niwahimize wananchi ,walezi na wazazi waweze kuwatuma vijana wao kujiunga katika vyuo vyetu vya mafunzo ya ufundi stadi. Pia niwahimize na waajiri kutumia wanafunzi wanaotoka katika vyuo hivi kuwaajiri kwani wanakuwa mahiri katika kazi zao na kushiriki kwenye uzalishaji moja kwa moja," amesema.

Vilevile, Maduku ametoa wito kwa vijana wanaomaliza mafunzo, kuanzisha shughuli zao binafsi kama ufundi seremala kwa kuzalisha bidhaa zao na kuuza.

“Nimefurahishwa sana na maonesho ya mwaka huu kwasababu yameonesha picha hali ya uzalishaji,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages