Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizundua ofisi ya
ardhi mkoa wa Mara. Kushoto kwa Waziri Lukuvi ni Mkuu wa mkoa wa Mara Adam
Malima na kushoto ni Bi Sophia Lugera mmoja wa wananchi wa kwanza kupatiwa hati
kwenye ofisi hiyo. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
William Lukuvi akizungumza huku akiwa amezungukwa na wananchi wa mkoa wa Mara walimfuata
kutaka kutatuliwa kero zao za ardhi wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa
wa Mara.
Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wamiliki wa ardhi ambao hati
zao za ardhi zinaishia miaka 33 kwenda ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa
hivi karibuni kuzihuisha ili kupatiwa za miaka 99.
Lukuvi ametoa kauli
hiyo jana mkoani Mara wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Mara ambayo ni
ofisi ya kumi na mbili kuzinduliwa ikiwa ni mfululizo wa kuzindua ofisi za
ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Alisema, kuna baadhi ya
wamiliki wa ardhi kwenye mikoa mbalimbali ambao viwanja vyao vimepimwa na
michoro kuidhinishwa lakini hati zao ni za miaka 33 na wamiliki hao
watakapoenda kuzichukua wanatakiwa kuziangalia ili zibadilishwe na kupatiwa hati za miaka 99.
‘’ Hati nyingi za wale
wamiliki ambao hawajazichukua zimekwisha muda wake, muende kwenye ofisi za
ardhi za mikoa, huko mtaelekezwa na Wasajili Wasaidzi wa ardhi katika ofisi
hizo namna ya kuzibadilisha ili mpatiwe za miaka 99’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, zaidi ya wamiliki wa ardhi 50,000 kwenye mkoa Mara
hawajachukua hati za ardhi wengi muda wa hati zao unaishia miaka 33 na kutaka kufika
ofisi za ardhi mkoa wa Mara kurekebishiwa na kupatiwa za miaka 99 ili iwe rahisi
kupata mikopo mikubwa .
Akizungumzia uzinduzi
ofisi ya ardhi mkoa wa Mara, Lukuvi alisema mkoa huo umekuwa na migogoro mingi
ya ardhi na kubainisha kuwa uzinduzi wa ofisi hiyo utawawezesha wananchi wa
Mara kumaliza migogoro kupitia ofisi hiyo badala ya kuipeleka migogoro kwake.
Waziri Lukuvi aliongeza
kuwa, pamoja na Wizara yake hapo awali kushughulikia kero na migogoro ya ardhi
lakini tatizo la kimfumo lilikuwa kubwa na kuweka wazi kuwa uzinduzi wa ofisi
za mikoa unakomesha kero ambapo sasa hakutakiwa na gharama yoyote kwa mmiliki
wa ardhi zaidi ya ile atakayolipia wakati wa kuomba hati.
‘’Mgogoro wa kimfumo
ulikuwa mkubwa zaidi na leo hii tumekomesha kero na hakuna gharama yoyote
mmiliki wa ardhi ataingia kufuatilia hati zaidi ya ile aliyolipa wakati wa
kuomba hati, serikali ya awamu ya tano imeondoa kero zote kwa wananchi kwenye
utawala wa ardhi’’ alisema Lukuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa
mkoa wa Mara Adam Malima alisema, ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko na
kero nyingi na kati ya malalamiko kumi na mbili anayopokea kwa siku sita yanahusiana
na ardhi na kusisitiza kuwa, mingi ya migogoro ya wananchi lazima nguvu hutumika
jambo alilolieleza kuwa linaongeza gharama za kiafya katika masuala ya matibabu na kubainisha kuwa uwepo ofisi ya ardhi
katika mkoa huo utarahisisha huduma katika sekta ya ardhi..
‘’ Kila malalamiko kumi
na mbili ninayopata ofisini kwangu sita ni ya ardhi na mengi yana sura ya
kijamii na hapa kuna neno la msamiati ukisikia vyesi ujue ni kesi’’ alisema
Malima.
Mmoja wa wakazi wa
Musoma aliyepatiwa hati katika uzinduzi ofisi ya ardhi Bi. Mara Sophia Lugera
alifurahishwa na usogezwaji huduma za ardhi mkoani Mara na kubainisha kuwa aliifuatilia
kwa muda mrefu hati yake iliyokuwa ofisi ya Kanda Mwanza na kusema, baada ya
kuipata hati ataitumia kuchukulia mkopo benki ili aendeleze biashara yake ya
ujasiriamali.
Katika
hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi alitembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa Hospitali ya
Rufaa ya mkoa wa Mara inayojulikana kama Mawalimu Nyerere Memorial Hospital
iliyopo eneo la Kwangwa Musoma mkoa wa Mara.
Akiwa katika mradi huo,
Lukuvi aliagiza kukamilika kwa jengo ya Huduma ya Mama na Mtoto kufikia mwisho
wa mwezi huu ili lianze kutumika kwa wananchi wa mkoa huo na Mikoa jirani.
Alisema, ujenzi wa
jengo hilo umechukua muda mrefu na anataka kuona sehemu ya jengo hilo
inakamilika kufikia julai 31 mwaka huu na Agosti mosi 2020 atamuagiza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwenda kuona kama agizo lake
limetekelezwa kama alivyoahidiwa.
Mhandisi na Msimamizi
wa mradi wa ujenzi wa Hosiptarli ya Rufaa mkoa wa Mara Renald Kazyoba alisema,
kimsingi sehemu ya ujenzi wa mradi huo sehemu ya Huduma ya Mama na Mtoto (Wing
C) itakamilika kama alivyoagizwa kwa kuwa kazi kubwa imefanyika.
No comments:
Post a Comment