HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 14, 2020

ZAIDI YA MAJANGILI 1300 WAKAMATWA KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA

 Na Mwandishi Wetu, Iringa

ZAIDI ya majangili 1300 wamekamatwa katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 kutokana na serikali ya awamu ya tano kuimarisha ulinzi wa wanyamapori.

Hayo yalielezwa leo na Afisa Uhifadhi Daraja la Pili Kitengo cha Ulinzi na Himasheria kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha David Mlay wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo kujionea mambo mbalimbali ya ujangili,uhifdhi na utalii.

Amesema mbali na majangili hayo lakini pia mifugo iliyoingia katika hifadhi hiyo zaidi ya 3000  nayo ilikamatwa.
Mlay amesema  wengi wa majangili waliokamatwa ni watanzania na sio raia kutoka nje ya nchi kutokana na kukatwa kwa mashina na mizizi ya uangili katika eneo hilo.
“Mitandao yote ya ujangili imekatwa kwani ili ujangili ufanyike lazima kuwepo na mtandao (Organised crime) lazima awepo jangili,mnununuzi na wasafirishaji”
“Tangu Serikali ya Rais John Magufuli aingie madarakani tunashukuru ujangili umepungua kwa kasi na wanyama wengi waliokuwa wanawindwa ni Faru na Tembo lakini kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama zinazozunguka hifadhi tumefanikiwa sana kuthibiti ujangili.

“Kabla Rais Magufuli hajaingia madarakani Tembo waliowindwa na kuuawa na majangili katika hifadhi hii walikuwa 30 lakini sasa hivi takwimu imeshuka na hakuna lakini wakati mwingine hutokea mara chache labda Tembo mmoja  na huyo hauawi na majangili ila baadhi ya wananchi ambao huwafukuza wakati wanyama hao wanapovamia mashamba yao na kula mazao”alisema Mlay
Mlay ameongeza kuwa baadhi ya majangili waliokamatwa ni pamoja na majangili wa kuvua samaki,kukutwa  na silaha,kuchimba madini ndani ya hifadhi na kufanya shughuli zingine zilizo kinyume na sheria ndani ya hifadhi..
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Tungamalenga kilichopo Kata ya Idodi wilayani Iringa Mkoa wa Iringa Abdulatif Ahmad amesema ushirikiano na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni mzuri lakini ni muhimu pia uongezwe zaidi ya ulipo sasa.

“Wanajitahidi sana hata kutuletea nafasi za ajira zinapotoka zikiwemo za ujenzi,kutoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori lakini tukiwaita kuna jangili wanafika mara moja lakini tukiwaita kuhusu wanyamapori kuvamia mashamba ya wananchi wanachelewa kufika”amesema Ahmad

Naye Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Tungamalenga Kamati ya Maendeleo ya Jamii Lucas Samwel amesema tangu wamenza ujirani mwema na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wamefanikiwa kujengewa Zahanati na majengo ya shule lakini changamoto kubwa ni uvamizi wa wanyamapori hasa Tembo katika mashamba ya wananchi na kuharibu mazao yao.

Kwa muda mrefu Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa kushirikiana na Shirikana la Internews wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali kwa ajili ya waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari za uhifadhi,utalii na ujangili wa wanyamapori kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Pages