HABARI MSETO (HEADER)


August 24, 2020

Sungaji wanavyofanikiwa kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji

Baadhi ya wakulima wa bonde la Mgongola, Mvomero waliowahi kujitokeza na kuelezea shuhuda kwenye moja ya Kamati Teule ya Bunge juu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji. (Picha kwa hisani ya mtandao).
 
 
 NA BETTY KANGONGA 
 

MIGOGORO ya ardhi hutokea sehemu mbalimbali nchini pindi sehemu mbili tofauti au zaidi zinapogombea haki ya kutumia kipande fulani cha ardhi. 

 

Wilaya ya Mvomero ni kati ya wilaya iliyokuwa ikikabiliwa na matatizo ya migogoro ya ardhi kwa miaka 15 iliyopita. 

 

Ambapo mgogoro mkubwa ni baina ya wakulima na wafugaji wanaoingia katika uhasama na kushindwa kuelewana baada ya kundi moja kuharibu mali ya mwingine. 

 

Ingawa kwa sasa hali imetulia ni matukio machache yanayojitokeza ambayo nayo yamekuwa yakidhibitiwa.

 

Kijiji cha KisalaKata ya Sungaji kilichopo katika Wilaya ya Mvomero kimekuwa kikikabiliwa na migogoro ya wakulima na wafugaji hasa kipindi cha kiangazi baada ya baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima.

 

Mwenyekitiwa Kijiji hicho Ramadhani Kilangilo anaeleza kuwa migogoro ya ardhi katika kijiji hicho imekuwa ikijitokeza zaidi katika kipindi cha Julai na kuendelea pamoja na kuwa kijiji kimejiwekea sheria ndogo ndogo za kudhibiti matukio hayo.

 

Anasema kuwa migogoro hiyo inachangiwa na wafugaji jamii ya wamasai kukosa malisho na kusababisha kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima hasa wale wanaolima mazao aina ya mahindi na mpunga kipindi cha kiangazi katika bonde la mgongola linalozunguka kijiji hicho.“Kipindi hiki cha Juni, Julai hadi Agosti ndiyo kunakuwa na tatizo kubwa la migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ,” anasema.

 

Anasema kuwa kipindi cha Januari hadi Machi hauwezi kupokea mgogoro wowote wa ardhi kwa kuwani kipindi cha mvua na wafugaji wanaogopa kuchunga kwa kuwa mifugo inawezakusombwa na maji. 

 

 “Kipindi cha masika hakuna mgogoro kwa kuwa wafugaji hawavuki kutokana na mito mingi kujaa maji hivyo wanaogopa mifugo yao inaweza kusombwa na maji,” anaeleza.

 

Kilangilo anaeleza kuwa, kijiji kimeunda sheria ndogo ndogo za kuhakikisha wanawachukulia hatua wale wote wanaovunja sheria za kusababisha kujitokeza kwa migogoro ya ardhi lakini baadhi ya wafugaji wanaotoka vijiji vya jirani wanashindwa kuziheshimu.

 

Anasema mara nyingi mgogoro unatokea pindi mkulima akibaini kuwa mali (mazao) yake yaliyoliwa hayalingani na faini aliyolipa mfugaji baada ya kuingiza mifugo na kula mazao.

 

“Tunaomba katika hili uongozi wa wilaya utafute ufumbuzi wa haraka maana haiwezekani mfugaji ameingiza ng’ombe katika shamba la hekari mbili na nusu kisha mfugaji anatozwa Sh.60, 000,…Malipo ambayo hayalingani kabisa na mali iliyoharibiwa, tunaomba kuwepo na usawa katika hili la sivyo hali hii inaweza kuzidi kuchochea migogoro ya ardhi katika kijiji chetu,” anasema.

 

Mwenyekiti huyo anasema, kuwa wakulima wanapaswa kuepuka propaganda zinazotolewa na baadhi ya wafugaji juu ya kuwepo kwa viongozi wa serikali ya kijiji wanaopokea fedha na kuruhusu wafugaji kupitisha mifugo katika mashamba ya wakulima.

 

“Hakuna kiongozi yeyote wa kijiji ambaye anaweza kushiriki katika kuteketeza wananchi wake, wafugaji wanapaswa kuacha kuwagombanisha viongozi wa vijiji na wananchi,…Wengi wao wanapokamatwa pindi wanapoingiza mifugo katika mashamba ya wakulima wanadai kuwa wameruhusiwa na viongozi wa vijiji jambo ambalo si la kweli ni kutaka kuwagawa wavijiji wasiuamini uongozi uliopo madarakani” anasema.

 

Anasema kuwa kutokana na ofisi ya kijiji hicho kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wanakijiji hivi sasa wamedhamiria kukutana na wafugaji wa kijiji cha Kambalaili kufanya mkutano wa ujirani mwema na kuangalia namna ya kuondokana na kero hiyo inayowatesa wakulima.

 

Naye mkazi wa kijiji cha Sungaji Issa Rajab anasema kuwa tatizo la migogoro ya ardhi katika kijiji hicho inaweza kuwa historia iwapo makundi ya wakulima na wafugaji wataamua kuheshimu sheria ndogondogo zilizoundwa.

 

“Mara nyingi mgogoro wa ardhi unatokea pale ambapo mifugo inaingizwa katika shamba la mkulima ambalo ndilo tegemeo la kaya husika,” anasema.

 

Anasema kuwa ingawa kwa sasa matukio ya migogoro ya ardhi sio mengi kama miaka mitano iliyopita hii ni kutokana na elimu inayotolewa na baadhi ya asasi za kiraia.

 

Mkazi huyo anasema kuwa bado wafugaji wachache wasiotii sheria hizo kuingiza mifugo katika mashamba lakini viongozi wa pande zote wanajaribu kutafuta ufumbuzi wa haraka ikiwa ni pamoja na kulipisha faini upande uliosababisha kujitokeza kwa mgogoro huo.

 

Mkazi mwingine Amina Sudi anakumbuka mgogoro wa ardhi uliotokea miaka mitano iliyopita ambapo ulimuathiri kiuchumi kwa kuwa hekari 16 za mpunga zililiwa na mifugo na kumsababisha kukosa chakula na hali ya kiuchumi kudorora.

 

“Kwa sasa migogoro imepungua kwa kuwa tunaweza kulima kwa amani ingawa ni mifugo michache inayopitishwa katika mashamba yetu ambayo nayo inaweza kudhibitiwa na serikali ya kijiji,” anasema.

 

Hata hivyo aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Florent Kayombo, alipata kufafanua kuwa, baadhi ya watendaji wa vijiji hivyo walikuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi.

 

“Hawa viongozi wa vijiji tuliwaondoa baada ya kubaini kuwa wamekuwa wakiitumia migogoro ya ardhi kujinufaisha kwani wakati wa migogoro hiyo walikuwa wakichangisha fedha wakulima na wengine walichangisha wafugaji na kudai wanakuja wilayani kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.” anasema.

 

Anasema kuwa walipobaini hilo tatizo hilo walipiga marufuku michango yote na kuweka sheria za kusimamia maeneo hayo huku wakilazimika kuitambua mifugo kwa kuipiga chapa zoezi ambalo hadi sasa bado limefanikiwa katika wilaya hiyo.

 

“Hadi sasa hatujatenga bado maeneo ya malisho ingawa hatutegemei ng’ombe kuongezeka kwani iliyopo hadi sasa ni 189, 000 katika wilaya yetu ambapo mfugaji mmoja huko Kambala anaweza kumiliki ng’ombe kuanzia 800 hadi 3000”, Naye aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali anasema, kwa sasa hakuna migogoro ya ardhi tofauti na miaka ya nyuma kuanzia 2012 hadi 2015 kwani kwa sasa inaweza kujitokeza kati ya mmoja kwa miezi hata sita ambapo huwezi kuitafsiri kama ni migogoro ya ardhi.

 

Anasema kuwa miaka ya nyuma kulikosekana kwa mipango bora ya matumizi ya ardhi vijijini, wanakijiji walishindwa kutenga maeneo ya makazi, mashamba, malisho na huduma za jamii ni sababu iliyosababisha kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo.

 

Pia baadhi ya viongozi kuhodhi maeneo makubwa huku wanakijiji wakipewa vipande vidogo vya ardhi na walio na mifugo kukosa malisho nayo ilikuwa chanzo cha kushamiri kwa migogoro ya ardhi katika kipindi hicho.

 

Pia Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Masuala ya Ardhi (HakiArdhi) imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu juu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao unaweza kuwa nyenzo ya kukuza usimamizi wa ardhi katika Wilaya ya Kilolo, Iringa. 

 

HakiArdhi inasema kuwa, mpango wa kijiji wa matumizi bora ya ardhi hutenga eneo la ardhi ya kijiji na kuwezesha uwekaji mipaka wa maeneo ya ardhi. 

 

Pia unajadili na kuamua juu ya matumizi na umiliki wa ardhi hii. Sera za mpango ya matumizi bora ya ardhi nchini Tanzania zilitungwa kufuatia mzozo unaokuwa unaohusu ardhi na maliasili na hitaji la usalama ulioboreshwa wa umiliki wa ardhi.

No comments:

Post a Comment

Pages