Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera akizungumza mbele ya Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni wakati akifungua Mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Na Asha Mwakyonde
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka watoa huduma ya habari mitandaoni kuhakikisha kuwa vyombo vyao haviwi chanzo cha kuleta taharuki ndani ya jamii kwa kutoa taarifa zisizokuwa na uhakika.
Akizungumza katika warsha iliyofanyika
jijini Dar es Salaam kwa watoa huduma hao, Mkurugenzi wa Tume hiyo Dkt. Wilson Mahera amesema njia muafaka ya kuepukana kusambaza taarifa zisizo kuwa sahihi ni kuzingatia misingi ya maadili ya kazi zao.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa Tume taari imeshafanya maandalizi mbalimbali ya uchaguzi na kwamba ili zoezi hilo lifanikiwe kwa kiwango kikubwa linategemea ushirikiano wa wanahabari.
"Nitoe rai kwenu watoa huduma za mtandaoni kutenda haki sawa kwa vyama vyote na kuhakikisha mnawapa wagombea nafasi ya kutangaza na kunadi sera na ilani za vyama vyao," amesema.
Aidha amesema NEC bado inaendelea kushughulikia rufaa walizokatiwa wagombea kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za uchaguzi na sio kufuata matakwa ya mtu.
Sambamba na hayo amesema katika maandalizi ya uchaguzi mwaka huu hakukuwa na marekebisho ya yeyote ya sheria za uchaguzi bali wamefanya maboresho ya kanuni za uchaguzi wa Rais na wabunge na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa (madiwani) kwa mwaka 2020.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Mawasiliano ya Tume ya Uchaguzi NEC Asina Omari amewataka wamiliki wa mitandao ya Kijamii kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinatoka katika vyanzo husiki.
"Ni muhimu kupata uhakika zaidi wa taarifa kabla ya kuandika taarifa ili kuepusha kusambaa kwa taarifa zisizo za kweli ambazo zinaweza kuleta taharuki ndani ya jamii" amesema Mwenyekiti Asina.
Aidha amesema watoa huduma ya Habari mitandaoni ya Kijamii wanajukumu la kuelimisha wengine na pia kujielimisha ikiwemo kujua msingi ya habari hizo pamoja na kufuata sheria na kanuni zake ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea pale ambapo jamii itapata taarifa ambazo
sio sahihi.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo mmiliki wa mtandao wa habari kutoka mkoani Kahama Shija feslishiani amesema elimu kwa waandishi wa habari za mitandao ya Kijamii ni muhimu kutolewa kutokana na idadi kubwa ya watu kupata taarifa mbalimbali kupitia mitandao hiyo.
Hata hivyo amesema elimu hiyo isipotolewa kwa wahusika inaweza kusababisha madhara makubwa kutokana na taarifa zake kusambaa kwa haraka na kwa idadi kubwa ya watu.
No comments:
Post a Comment