HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 12, 2020

Waziri Mkuu aipongeza NMB kuchangia Mil. 100 wagonjwa wa saratani


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi hundi ya sh. Milioni 100 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Maseru, (kushoto) wakati alipohitimisha  Mbio za NMB Marathon kwenye viwanja vya Mlimani City jijini Dar es salaam, Septemba 12, 2020. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji) Angellah Kairuki, wa tatu kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, wa pili kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sanlam  East Africa, Julius Magabe na wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dkt.Edwin Mhede. Fedha hizo zilizotolewa na Benki ya NMB zitatumika kuwasaidia watoto wenye ugonjwa saratani wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Badhi ya washiriki wa Mbio za Kilomita 5 za NMB Bima Marathon 2020, wakianza mbio hizo jijini Dar es Salaam.

 

 

NA MWANDISHI WETU

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameipongeza Benki ya NMB kwa kutoa kiasi cha Sh. Mil. 100 kuchangia matibabu ya watoto wenye saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), huku akikiita kitendo hicho kuwa kinachopaswa kuigwa na wadau wa afya nchini.

 

NMB imetoa kiasi hicho Jumamosi Septemba 12, kikitokana na ada ya usajili wa washiriki wa Mbio za Kilomita 5 za NMB Bima Marathon 2020, zilizodhaminiwa na benki hiyo, zikilenga kutoa elimu ya bima, sambamba kuhamasisha mazoezi ya viungo kwa jamii.

 

Akizungumza wakati wa kupokea hundi ya kiasi hicho, Majaliwa alisema licha ya jitihada za Serikali katika kumaliza changamoto kwenye Sekta ya Afya, bado kuna uhitaji mkubwa miongoni mwa wagonjwa, hospitali na vituo vya afya na kwamba NMB imeliona hilo na kujitoa kusaidia.

 

‘‘Niwapongeze NMB kwa kuyatoa makusanyo ya Sh. Mil. 100 na kuchangia matibabu ya watoto wanaougua saratani. Hii maana yake ni kuwa mnaungana na kasi ya Serikali ya Rais John Magufuli sio tu katika kutatua changamoto za afya, bali pia kuhamasisha mazoezi.

 

‘‘Jamii isiishie hapa, mahitaji ya kitiba kwa wagonjwa mbalimbali ni mengi, kama ilivyo kwa hospitali zetu, vituo vya afya na zahanati zetu. Ndio maana natoa wito kwa wadau wa afya, zikiwemo taasisi na mashirika, kuiga mfano huu walioufanya NMB,’’ alisema Majaliwa.

 

Waziri Mkuu Majaliwa  Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa Hospitali za Rufaa zinazotoa huduma kwa wagonjwa  wenye Saratani kutenga wodi  maalumu kwa ajili ya watoto wenye saratani.


Aliongeza kuwa mbio hizo zimekuja wakati muafaka, kwani zinaendana na mwezi maalum wa uhamasishaji na uelewa kuhusu magonjwa ya saratani kwa watoto duniani na kwamba matumaini yake ni kuwa hamasa iliyofanywa na NMB, itakuwa na mafanikio makubwa kwa jamii.

 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, mbio za NMB Bima Marathon ni zao la ushirikiano wa kikazi baina ya NMB na mashirika ya bima nchini, ulioanzia Februari mwaka huu – pale benki hiyo ilipozindua huduma ya NMB BancAssurance.

 

‘‘Kwa ushirikiano huu, NMB sasa tunaweza kusambaza na kuuza bima kupitia matawi yetu yote na hivyo kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa huduma za Bima kwa urahisi zaidi. Lengo kuu ni kusaidia kuleta huduma za bima karibu na Watanzania.

 

‘‘Kimsingi huduma hii imesaidia kusisimua soko la bima kwa kiwango kikubwa, ambako Watanzania hata wa vijijini, ambako huduma za NMB zinapatikana, sasa wanaweza kupata huduma za Bima kwa urahisi na haraka zaidi,’’ alisema Zaipuna.

 

Alitoa wito kwa wadau nchini kuunga mkono jitihada za Serikali na benki yake katika kuyajali makundi yenye uhitaji, kwa kujenga utamaduni wa kuchangia gharama za matibabu, sambamba na kuhamasisha umuhimu wa bima za afya kwa jamii.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru, aliishukuru NMB kwa mchango wao kwa watoto wanaougua saratani na kwamba anaamini washiriki wa NMB Bima Marathon, watakuwa mabalozi wema wa utamaduni wa kusaidia makundi maalum.

No comments:

Post a Comment

Pages