HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 02, 2020

ASILIMIA 70 YA WAGONJWA WANAOFIKA JKCI WANAKABILIWA NA SHINDIKIZO LA DAMU

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesema kuwa asilimia 70 ya wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo wanakabiliwa na tatizo la Shindikizo la damu.

JKCI imesema tatizo hilo linaongoza kwa kushika namba moja kwa idadi kubwa ya wagonjwa katika taasisi hiyo.

Hayo yote yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Samweli Rweyemamu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Tanganyika Packers kwenye Maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani ambayo hufanyika Septemba 29, kila mwaka.

Dk. Rweyemamu amesema wapo pia wagonjwa wengine wanaokabiliwa na tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye moyo ambayo husababisha kifua kuuma.

“Kuna wengine wanaohitaji upasuaji tunaona idadi inaongezeka kila siku, kwa mfano wale ambao mishipa ya damu inaziba tunawazibua kwa upasuaji mkubwa (open heart surgery) au ule mdogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.

“Tunaona wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wanaongezeka, mwaka jana hadi Desemba, kwa kutumia mtambo wa Cathlab tuliwachunguza na kuwatibu wagonjwa 1409 hii ni idadi kubwa, wagonjwa hawa hapo kabla tulikuwa tunawapa rufaa kwenda nje ya nchi,” ame: sema.

“Sasa hatujui kama wanaongezeka kwa sababu tunatangaza kila siku, wanajitokeza kuja hospitalini, tuna uwezo wa kuchunguza na kutibu, lakini kwa ujumla tunaweza kusema matatizo yameongezeka,” alisema.

Dk. Rweyemamu alitoa mfano, hivi karibuni katika Wilaya ya Temeke, Viwanja vya Zakheem tulipima watu 103 asilimia 18 walikuwa na shinikizo la damu, wengine moyo umetanuka, kati yao wagonjwa 21 walionekana wana matatizo ya moyo.

“Tulienda pia Viwanja vya Mwembe Yanga na kupima watu 150 asilimia 22 walionekana wana magonjwa ya moyo kati ya hiyo asilimia 22, asilimia 19 walikuwa na shinikizo la damu la juu la damu,” alisema.

Aliongeza “Utaona ni idadi ndogo tunapima lakini tafiti zilizofanyika Dar es Salaam, zinaonesha karibu asilimia 30 wana shida ya shinikizo la damu, sasa ukiwa na shinikizo la damu ni ‘risk factor’ ya kuziba kwa mishipa ya moyo kuziba hatimaye utafika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tukuzibue kwa vifaa maalum.

Dk. Rweyemamu amesema mtu akiwa na shinikizo la damu moyo hutanuka na kuwa na dalili za moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) kwa hiyo asilimia kubwa ya matatizo ya moyo kwa watu wazima yanaanza na shinikizo la damu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi amesema magonjwa ya moyo huchangia karibu asilimia 31 ya vifo vyote duniani na kwamba takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kila mwaka takriban watu milioni 18 hufariki dunia kwa magonjwa hayo.

“Ni tatizo linaloonekana kuongezeka, takwimu zinaonesha katika kila mwanamke mmoja kati ya wanne na mwanaume mmoja kati ya watano wanakabiliwa na tatizo la shinikizo la damu,” alibainisha.

Aliongeza “Magonjwa ya moyo ni kati ya magonjwa yasiyoambukiza, ambayo kinga ni rahisi kuliko tiba, ndiyo maana WHO pamoja na Jumuiya ya Magonjwa ya Moyo Duniani baada ya kuona yanaongezeka wakaamua kuanzisha Siku ya Moyo Duniani.

“Leo (jana) hapa tunaelimisha jamii jinsi ya kujikinga, tunafanya uchunguzi na matibabu na wengine tunawapa rufaa kuja kule kwenye taasisi yetu kwa matibabu zaidi.

“Watu wanapaswa kuzingatia unywaji wa pombe kwa kiasi, kuacha uvutaji wa sigara, kula vyakula vinavyofaa, wazingatie kunywa dawa wanazoandikiwa (waliokutwa na matatizo haya) na wafanye mazoezi, wapunguze uzito uliopitiliza.

“Haya ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wa mtu bila gharama,” alisisitiza Prof. Janabi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema JKCI kwa siku huwa wanaona takriban wagonjwa 300 hadi 400 na kwamba tangu wameanza 2015 hadi sasa tayari wameshaona wagonjwa 350,000 na kuwafanyia upasuaji wa moyo wagonjwa 6,000.

“JKCI tupo mstari wa mbele kutoa elimu ili watu waepuke magonjwa haya,” alisisitiza Prof. Janabi.

Awali, Mratibu wa Tiba wa Manispaa ya Kinondoni kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dk. Omary Mwangaza amesema kipindi cha Julai na Agosti, mwaka huu katika vituo vya kutolea huduma za afya, waliibua wagonjwa wapya zaidi ya 600 wanaokabiliwa na magonjwa yasiyoambukiza.

“Shinikizo la damu na kisukari ni magonjwa yaliyokuwa yakiongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa, wagonjwa wote hawa tumewaingiza kwenye mfumo wetu wa matibabu,” alibainisha.

Amesema upimaji huo wa magonjwa ya moyo bila malipo uliofanyika katika maadhimisho ya siku ya moyo Duniani umewasaidia wananchi wengi kupata huduma kwani kuna ambao wamepewa dawa za kutumia, ushauri na wengine rufaa za moja kwa moja kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

No comments:

Post a Comment

Pages