HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 29, 2020

Siasa, uvunaji haramu vikwazo USMJ Darajani


Ofisa Misitu Wilaya ya Liwale, Nassoro Mzui akielezea utekelezaji wa mradi wa USMJ kijiji cha Darajani, Kata ya Mihumo. Kushoto ni Ofisa Sera na Uraghibishaji wa MJUMITA, Elida Fundi.

Wanakijiji wa Darajani wakiwa wanafatilia kwa makini kuhusu USMJ kijijini kwao.

 

NA SULEIMAN MSUYA, LIWALE


TOFAUTI za kisiasa, uvunaji haramu wa rasilimali misitu katika Msitu wa Narungombe zimetanjwa kuwa ndio sababu kubwa ya kijiji cha Darajani kuchelewa kutekeleza Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).

Msitu wa Narungombe wenye ukukwa kwa hekta 5,033 ni sehemu ya Msitu wa Angai uliopo wilaya ya Liwale mkoani Lindi.

Taarifa hizo za kukwama kwa miradi ya USMJ, zimetolewa na wananchi wa kijiji hicho mbele ya waandishi wa habari za mazingira, uhifadhi na misitu waliokuwa katika ziara ya kujifunza na kuona mafanikio na changamoto za usimamizi shirikishi wa misitu vijijini.

Waandishi hao kutoka vyombo mbalimbali waliambatana na maofisa wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) ambayo yanatekeleza Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFOREST) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).

Akizungumzia kukwama huko kwa  miradi ya USMJ, Mzee wa kijiji hicho Abdulrahman Ngokwe amesema walikataa mradi huo kupitia vikao halali vya kijiji kutokana na uelewa tofauti na mwingiliano wa kisiasa.

Amesema katika kipindi hicho Serikali ya kijiji kilikuwa chini ya Chama cha Wananchi (CUF) ambao amedai kuwa walikuwa wakipinga mambo mazuri.

Mzee Ngokwe amesema pia walikuwepo watu wachache ambao walikuwa wanavuna kwa njia haramu hivyo kutumia wingi wao kuwagawanya ili wao waweze kunufaika.

"Sisi tumakataa mradi huu kwa sababu za kisiasa na uvunaji haramu hali ambayo imeturudisha  nyuma na sisi kati ya vijiji vinne vya kata ya Mihumo tumebaki nyuma kimaendeleo," amesema.

Amesema baada ya kupata elimu na kuona manufaa ya majirani zao wa Likombora, Turuki na Mihumo ambao wamefanikiwa.

Zaituni Likwata Mwenyekiti wa Kamati ya  Maliasili amesema wamejipanga kusimamia kwa makini ili waweze kumufaika na msitu wao.

Likwata amesema wanatarajia kupitia Msitu wa Narungombe wanafanikiwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa shule, kupata vitendea kazi vya ulinzi wa misitu.

Aidha, amesema elimu waliyopata imechochea wanawake wengi kushiriki kwenye USMJ.

Mussa Abdallah amesema pamoja na siasa kukwamisha USMJ uelewa ulikuwa mdogo ila sasa wapo vizuri.

"Sisi tulifanya ujinga ila kwa sasa tupo pamoja kushiriki kikamilifu kulinda msitu wetu na kuundeleza," amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha  Darajani Hamisi Mbanila amesema Serikali ya kijiji ipo tayari kushiriana na wananchi na serikali  yote ili misitu iwe na tija kwa jamii ya Darajani.

"Elimu imesaidia kila mwanakijiji ni mlinzi wa msitu kwani maendeleo ya vijiji jirani yanawaumiza," amesema.

Ofisa Misitu wa Wilaya ya Liwale, Nassoro Mzui amesema wilaya yao ina vijiji 27 vyenye misitu ya asili ambapo vijiji 23 vipo ndani ya Msitu wa Angai na vijiji vinne vipo nje ya Msitu wa Angai.

Amesema USMJ Liwale inatekelezwa na Program ya Mnyororo wa Thamani  wa Mazao ya Misitu (FORVAC) na CoFOREST.

Amesema pamoja na mafanikio ambayo yamepatikana kupitia miradi hiyo bado ipo changamoto ya ukubwa misitu hivyo ulinzi kuwa hafifu.

Mzui amesema Halmashauri ya Liwale inajivunia kwa kuondoa idadi ya vijiji tegemezi kutoka bajeti ya wilaya.

Amezitaka wilaya nyingine nchini kuhamasisha USMJ kwani ni mfumo rafiki na endelevu kwa misitu ya vijiji.

Ofisa Sera na Uraghibishaji kutoka MJUMITA amesema wameamua kuzunguka na waandishi ili waone na kujifunza faida zilizopo kwenye USMJ.

"Vijiji vinanufaika sana kiuchumi, kimaendeleo, kijamii huku uhifadhi ukiwa mzuri tofauti na vijiji ambavyo havina USMJ," amesema.

Fundi ameziomba taasisi mbalimbali kwenda kwenye vijiji ambao vina misitu ya asili na kusambaza elimu ya USMJ ili kuweza kuokoa zaidi ya hekta milioni 17 kati ya milioni 22 za misitu ya vijiji.

Amesema iwapo waandishi wataweka bayana mafanikio ya USMJ watunga Sera na wafanya maamuzi watajua umuhimu wake.


No comments:

Post a Comment

Pages