Mkimbizi kutoka DRC Congo, Ebengo Waluta, akielezea namna alivyojikuta anakuwa mkimbizi mbele ya washiriki wa semina iliyoandaliwa na Diginity Kwanza.
Ofisa Hifadhi na Sheria wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Asnath
Barnabas akitoa mada kuhusu Sheria ya Wakimbizi ya mwaka 1998 kwa wa washiriki wa semina iliyoandaliwa na Diginity Kwanza.
NA SULEIMAN MSUYA
KATIKA
kuhakikisha Watanzania wanaelewa historia ya nchi yao katika kupokea na
kuhifadhi wakimbizi wadau mbalimbali wanashirikiana na Serikali
wanaandika kitabu kitakacho elezea historia hiyo kwa miaka 60 iliyopita.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Diginity Kwanza Janemary
Ruhundwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari na wadau kutoka
Asasi za Kiraia (CSOs) katika warsha ya siku mbili iliyofanyika jijini
Dar es Salaam.
Ruhundwa
amesema Diginity Kwanza inashiriki mchakato huo kama mratibu lengo
likiwa ni kuhakikisha historia ya zaidi ya miaka 60 ya ushiriki wa
Tanzania kupokea na kuhifadhi wakimbizi inawekwa kwenye maandishi na
usahihi.
"Tumewaita nyie
waandishi wa habari na CSOs ili muelewe kinachofanyika kwenye mchakato
wa kuandika kitabu hiki ambacho kitaonesha miaka 60 ya ushiriki wetu
kwenye kupokea na kuhifadhi wakimbizi.
Kitabu
hiki kitandikwa na sisi Watanzania wenyewe hivyo tumeamua kukutana na
Watanzania wote ambao watakuwa na taarifa kuhusu wakimbizi," amesema.
Amesema wao kama Diginity Kwanza wanaamini historia hiyo itasaidia jamii kuelewa mchango wa nchi kwenye eneo hilo.
"Pamoja
na juhudi za Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo pia eneo la
wakimbizi Tanzania imefanya mambo makubwa sana ndio tunataka kuyaanisha
kwenye kitabu sasa," amesema.
Ruhundwa
amesema matarajio yao ni kitabu hicho cha miaka 60 ya kupokea na
kuhifadhi wakimbizi kinakamilika mwishoni mwa mwaka 2021.
Mkurugenzi huyo amesema watahakikisha kitabu hicho kinaandikwa kwa lugha inayoeleweka kwa Watanzania wote.
"Naomba
ndugu zangu waandishi mtumie kalamu zenu kuandika habari za wakimbizi
kwa kina ili tuwe na kizazi chenye uelewa kwenye eneo hilo," amesema.
Ruhundwa
amesema awali walifikiria kuandika kitabu cha kutumika vyuoni lakini
baada ya mijadala wameona umuhimu wa kuwepo kitabu chenye kuhusisha
Watanzania wote kwanza.
Amesema
kumekuwepo na taarifa za utafiti kuhusu wakimbizi ambazo zinaandikwa na
watu kutoka nje hivyo ni wakati muhimu kutumia wazawa kuandika historia
hiyo muhimu kwa nchi.
Emmanuel
Mgala wa Kituo cha Kusimamia, Mazingira na Utawala Bora amesema kitabu
hicho kitafungua watu wengi kuhusu ukimbizi nchini hasa wale ambao
wanaamini Tanzania haigharamiki kuhifadhi.
"Kitabu
hiki ni fursa muhimu kwani watu watajua ukweli wa halisi ya nchi yao
kwenye eneo la wakimbizi ambalo linachukuliwa kama jambo la kawaida,"
amesema.
Kwa upande wake
Ruth Ndagu wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC),
amesema kitabu hicho kitakuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania ambayo
imekuwa ikipokea wakimbizi kwa miaka 60 na zaidi.
"Jamii
itapata mwanga kuhusu dhana ya wakimbizi lakini pia tutaendelea kutunza
amani yetu kwani ukimbizi sio jambo zuri," amesema.
Ndagu amesema kitabu hicho kitafungua ukurasa mpya kwa mashirika ya kimataifa kuongeza misaada katika eneo hilo.
Naye
Saimon Samitei Meneja Mwandamizi wa Miradi Shirika la Relief to
Developing Society (REDESO), amesema uandishi wa kitabu hicho kwa sasa
ni wakati muafaka.
Amesema wadau wanapaswa kuunga mkono uandishi wa kitabu hicho ili kusaidia jamii ya Kitanzania kupata elimu.
Samitei
amesema mchango wa Tanzania katika kuhifadhi wakimbizi ni mkubwa sana
hivyo kitabu kinapaswa kuanisha kila kitu kwa kina.
Akizungumzia
hisitoria ya miaka 60 ya kupokea na kuhifadhi wakimbizi nchini Ofisa
Tawala Mkuu, Usimamizi wa Kambi na Makazi kutoka Idara ya Huduma kwa
Wakimbizi, Stephen Msangi amesema imepitia changamoto na mafanikio hivyo
kitabu hicho ni muhimu kuandikwa.
Msangi
amesema kwa miaka 60 sasa Tanzania imepokea wakimbizi kutoka nchi ya
Malawi, Msumbiji, DRC Congo, Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya hivyo
historia hiyo ikiandikwa iweze kuanisha uhalisia huo.
"Tumepokea
wakimbizi wengi sana na wengine wameomba uraia wamekuwa Watanzania ila
wengi werudi katika nchi zao haya yote yanapaswa kuwa kwenye kitabu,"
amesema.
Aidha,
amesisitiza kitabu hicho kianishe changamoto ambazo nchi inakutana nazo
katika kuwahifadhi wakimbizi ili Watanzania wajue.
Ofisa
Hifadhi na Sheria wa Idara hiyo, Asnath Barnabas amesema kitabu hicho
kitafungua ukurasa mpya kwenye eneo la wakimbizi nchini.
No comments:
Post a Comment