Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ)
hakiridhishwi na mwenendo wa hukumu zinazotolewa na Mahakama ya Wete
Mkoa wa kaskazinia Pemba kwa kuwaachia huru watuhumiwa au kuwapa adhabu
ndogo dhidi ya makosa ya ukatili wa kijisia kwa watoto.
Hivi
karibuni TAMWA Zanzibar imepokea taaarifa kwamba mtuhumiwa Salim Khamis
Ali maarufu “Panga la Shaba” (43) mkaazi wa Taifu shehia ya Kinyasini
aliyembaka mtoto wake wa kumzaa huko Pemba ameachiwa huru kwa madai
kuwa taarifa za daktari zimeonesha kwamba mtoto huyo ni mzoefu kwa
maana ya kuwa ameshatenda tendo la ngono hapo awali.
Tukio
hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi Wete tarehe Desemba 6/ 2019
na kufunguliwa jalada namba IR471/2019 ambapo jalada hilo lilieleza
kwamba Salim Khamis Ali anatuhumiwa kumbaka mtoto wake wakike aliye
chini ya umri wa miaka 13.
Kwa
mujibu wa hakimu wa Mahakama ya Wete Mkoa Kaskazini Pemba, Abdalla
Yahya Shamhuni, ni kwamba mtuhumwa alitenda kosa Novemba 30, 2019 saa
3:00 usiku katika eneo la Taifu, ambapo bila ya halali mtuhumiwa huyo
alimuingilia mtoto huyo huku akijua kuwa ni mtoto wake wa kumzaa, jambo
ambalo ni kosa kisheria kwa mjibu wa kifungu cha 143 (1) (4) cha Sheria
namba 6 ya mwaka 2018, Sheria ya Zanzibar ambapo kesi hiyo ilipewa
nambari RM 4/2020.
Hakimu
huyo alibainisha kwamba baada ya kukamilika kwa upelelezi kesi hiyo,
Mahakama imemuachia huru mtuhumiwa tarehe Desemba 7/2020 kwa kile
kinachodaiwa ushahidi wa daktari ulionyesha kuwa muathirika aliwahi
kuingiliwa hapo awali.
“Katika
maelezo yake daktari alieleza kuwa muathirika ni mzoefu. Hivyo basi
baada ya kupitia vyema ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka
mahakama imeona kwamba mtuhumiwa si mkosaji wa kosa hilo na inamuachia
huru chini ya kifungu cha 220 cha sheria namba 7 ya mwaka 2018 sheria ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema Shamhun”.
TAMWA
ZNZ inaomba mahakama na Serikali kuangalia athari inayowapata
waathirika kabla ya kutoa hukumu, kwani kitendo cha baba mzazi
kumwingilia mwanawe ni kosa la jinai hasa kwa vile mtoto huyo ni mdogo
anayestahiki kulindwa na taifa.
Kwa
mujibu wa sheria za nchi ikiwemo sheria namba nne ya 2005 ya kumlinda
mtoto mwari na watoto wenye mzazi mmoja na sheria ya adhabu ya namba 7
ya 2018 ni kwamba mtoto chini ya miaka 18 hana ridhaa ya kufanya maamuzi
ya kimapenzi bila ya ushawishi na kubakwa, hivyo baba mzazi huyo
anastahiki kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Hivyo
hatua ya kumuachia huru Mzazi huyo inapaswa iangaliwe tena upya kwani
inaweza kurudisha nyuma juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia pamoja na
kujenga taifa lenye vijana waliosoma na wenye kujiamini katika kuleta
maendeleo ya nchi.
Kuwaachia
huru watuhumiwa kama hawa inapelekea ongezeko la matukio ya
udhalilishaji hapa Zanzibar kwasababu watuhumiwa hawaogopi na kuendeleza
vitendo hivyo vinavyoathiri maisha ya watoto na wanawake kwa jumla.
Aidha
TAMWA,ZNZ inapenda pia kuishauri Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake katika kuandika ripoti za kidaktari
ili kuwa nyeti katika masuala ya kijinsia na hivyo kutokuita watoto
wadogo wazoefu kwenye mausla ya kujamiiana.
No comments:
Post a Comment