HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 10, 2021

MEYA UBUNGO AMPONGEZA MKURUGENZI KWA USIMAMIZI MADHUBUTI MIRADI INAYOENDELEA KUTEKELEZWA

 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imesema kuwa imefikia hatua nzuri za Ujenzi wa Madarasa unaoendelea katika Shule ya Msingi Kingo'ngo iliyopo ndani ya manispaa hiyo.


Aidha imebainisha kuwa itaendelea na kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya katika kata zilizomo ndani ya manispaa hiyo lengo likiwa kuwaondolea adha wananchi kufuata huduma mbali kwa kuwasogezea karibu ikiwemo Kata ya Makurumla kwa kadri bajeti ya manispaa itakavyokidhi.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Beatrice Kwai katika Kikao cha Baraza la Madiwani ambapo alisema ujenzi wa madarasa katika shule hiyo unaendelea na kwamba matumaini yao ni kukamilisha ndani ya muda ili wanafunzi waendelee na masomo katika mazingira rafiki.

" Tunaendelea na ujenzi wa madarasa tunakimbizana na muda tumalize kwa wakati viongozi wanaendelea kuwajibika lengo tumalize kwa wakati wanafunzi wapate mazingira rafiki ya kuendelea na masomo," alisema Mkurugenzi Beatrice.

Alibainisha kuwa manispaa hiyo imejipanga kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo kulingana na bajeti itakavyopangwa kutekeleza miradi iliyopo na mingine itakayopendekezwa na madiwani katika kata zao husika.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Japhar Nyaigesha amempongeza mkurugenzi huyo kwa usimamizi madhubuti wa miradi inayoendelea kutekelezwa katika kata za manispaa na kwamba wamejipanga kuboresha huduma katika sekta zote.

Meya Nyaigesha aliwakumbusha watendaji wa Idara ya Mipango Miji kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha hakuna migogoro ya ardhi inayokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo ya manispaa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages