HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 23, 2021

UTT- AMIS na fursa zake

Pesa hukua! lakini ili ikue ni kuna mambo lazima yafanyike. Moja wapo ni kuwekeza katika masoko ya fedha na mitaji, mfano ni kununua hisa za makampuni mbalimbali na kuwekeza kwenye hati fungani.

Tuelewane taratibu!

Hisa ni sehemu au asalimia ya umiliki wa kampuni. Kama kampuni ina hisa 1,000,000 na mwekezaji anamiliki hisa 10,000, mwekezaji huyu anamiliki 1% ya kampuni hiyo. Stahiki za mwenye hisa ni pamoja na kushiriki katika kutoa maamuzi ya kampuni na kupata gawio la faida. Ana haki pia ya kuuza hisa zake kwa faida pale ambapo kuna ongezeko la thamani ya hisa.

Hati fungani ni hati ya deni ambalo kampuni au serikali huwakopa wawekezaji kwa makubaliano maalumu na kuwalipa riba na marejesho baada ya kupevuka kwa hatifungani hiyo. Mwenye hatifungani anastahili kulipwa riba (kwa kawaida ni kila miezi sita) na kurudishiwa mtaji wake ikishapevuka. Pale ambapo kampuni inafilisika, wanaomiliki hatifungani wana haki ya kulipwa pesa zao kabla ya wale wanaomiliki hisa.

Twende kwenye point sasa!

Serikali ilibaini kuwa si kila anayetamani kuwekeza ana pesa ya kununua hisa au kuwekeza katika hati fungani. Hivyo, iliunda mifuko wa uwekezaji wa pamoja inayoendeshwa na UTT Asset Management and Investor Services Plc (UTT AMIS).

Uwekezaji wa pamoja unaweza kufanywa na mtu binafsi, kampuni au taasisi. Upekee wake ni kuwa unatoa fursa ya uwekezaji hata kwa wenye fedha kidogo kwa mfumo wa kununua vipande. Ili kuelewa tutumie huu mfano. Unanunua vipande vya UTT AMIS, wao wanachukua hiyo pesa yako pamoja na pesa za wawekezaji wengine na kupata mitaji mikubwa ambayo wanaiwekeza. Faida itakayopatikana itagawanywa kulingana na kiasi ulichowekeza, kama faida ni 10% ya uwekezaji wote, kila mmoja atapata 10% ya pesa yake kama faida. Unaweza kuuza vipande vyako muda wowote lakini, kadri muda unavyokwenda ndio pesa yako hukua zaidi kwa sababu, ile faida inayopatikana nayo huwekezwa na kuzaa faida.

Mifuko ya Uwekezaji

UTT AMIS inaendesha mifuko sita ambayo inatofautiana katika vigezo na manufaa. Vigezo vikuu ni malengo ya mwekezaji, muda anaotaka kuwekeza, anavyoweza kubeba hatari za uwekezaji, faida anayotarajia, uharaka wa kupata fedha  na umri wa mwekezaji.
 
Mfuko wa Umoja

Mfuko huu unawekeza kwenye masoko ya mitaji kama vile hisa zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es salaam kiwango kisichozidi (50%) na masoko ya mengine ya fedha yenye sifa tofauti kwa kiwango kisichopungua 50%. Hivyo ni Mfuko mzuri kwa uwekezaji wa muda mrefu. Kiwango cha chini kuanza kuwekeza ni shilingi 6,500 kwa sasa.

Mfuko wa Wekeza Maisha

Mfuko huu ni mpango wa wazi na wa muda mrefu unaokusudia kukuza mtaji na kwa wakati huo huo kutoa kinga ya bima ya maisha, bima ya ajali/ulemavu wa kudumu na gharama za mazishi. Mpango wa uwekezaji katika Mfuko huu ni miaka 10.
Mfuko una mipango ya uwekezaji ya aina mbili; mpango wa uwekezaji kwa awamu na uwekezaji wa mkupuo. Kiwango cha chini kwa uwekezaji kwa miaka kumi ni Shilingi Milioni 1.  Kiwango cha chini cha uwekezaji wa awamu ni Sh.8,340/= kwa kila mwezi.


Mfuko wa Watoto

Mfuko huu unaokusudia kukuza mtaji kwa muda mrefu kupitia uwekezaji wa pamoja kwa kuwekeza kwenye hisa zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa na dhamana. Uwekezaji unafanywa kwa jina la mtoto aliye chini ya miaka 18 na ni kwa manufaa ya mtoto huyo. Mfuko unatoa fursa mbili za uwekezaji; malipo ya ada ya masomo (Scholarship), na ukuzaji wa mtaji. Kiwango cha chini cha kuwekeza ni Sh.10,000 na kiwango cha chini cha uwekezaji wa nyongeza ni Sh.5,000. Uuzaji wa sehemu ya vipande au vyote unaruhusiwa pale mtoto mnufaika anapotimiza miaka 12 (wastani wa umri wa kujiunga na elimu ya sekondari nchini) iwapo wakati wa kuanza kuwekeza mtoto alikuwa na umri chini ya miaka 12.


Mfuko wa Jikimu


Mfuko huu unatoa fursa mbili za uwekezaji; gawio kila baada ya robo mwaka, gawio kila mwaka  na mpango wa kukuza mtaji. Kiwango cha chini cha kuwekeza ni 2,000,000  kwa mpango wa mapato ya robo mwaka, 1,000,000 kwa mpango wa gawio kwa mwaka na 5,000 kwa mpango wa kukuza mtaji.


Mfuko wa Ukwasi

Dhumuni la mfuko huu ni kutoa faida ya uhakika kutegemeana na hali ya soko. Mfuko huu unawekeza kwenye dhamana zenye kutoa mapato ya kudumu na masoko ya fedha.Hivyo ni mzuri kwa wawekezaji wenye malengo ya muda mfupi hadi mrefu na ambao hupenda hatari ndogo za uwekezaji. Kiwango cha chini cha uwekezaji wa mwanzo ni Shilingi 100,000  na uwekezaji unaofuatia kiwango cha chini ni shilingi 10,000.

Mfuko wa Hati Fungani
Huu ni mfuko unaowekeza katika hati fungani za serikali, makampuni na katika masoko ya fedha. Hivyo faida ni uhakika kulingana na hali ya soko. Kiwango cha chini cha kuanza kuwekeza ni  50,000 kwa mpango wa kukuza mtaji ,10,000,000 kwa mpango wa gawio kila mwezi na shilingi 5,000,000 kwa mpango wa gawio kila baada ya miezi sita.Nyongeza kwa mipango yote mitatu shilingi 5000 au zaidi.


Mazuri ni mengi!
Ni vigumu kuyaelezea hapa. Kikubwa ni kwamba, uwekezaji huu ni rahisi. Unaweza kuwekeza kwa kutumia simu kwa kubonyeza namba *150*82# au akaunti ya benki. Kufahamu zaidi, tembelea www.uttamis.co.tz au piga bure; 0754 800 544 255, 0715 800 544 na 0782 800 455. Ukiona tawi lao, zama ndani watakupa taarifa zote.

No comments:

Post a Comment

Pages