Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka viongozi wa Tume ya Madini kufanya kazi kwa kujiamini huku wakifuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.
Waziri Biteko
ametoa kauli hiyo leo tarehe 24 Februari, 2021 kwenye ufunguzi wa
mafunzo ya siku mbili kuhusu mfumo wa wazi wa mapitio na tathmini ya
utendaji kazi(OPRAS) yanayoshirikisha Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa
Madini Wakazi wa Mikoa wa Tume ya Madini jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
katika mafunzo hayo yanayotolewa na Tume ya Utumishi wa Umma, Waziri
Biteko amewataka viongozi kuhakikisha wanafanya kazi kwa kujiamini na
kutatua changamoto badala ya kufanya kazi kwa kusubiri maelekezo kutoka
juu.
"Ni vyema
mkahakikisha mnafanya maamuzi yaliyopo ndani ya uwezo wenu kwa
kuzingatia Sheria ya Madini na kanuni zake badala ya kusubiri maelekezo
kutoka kwa viongozi wa juu wa Wizara", amesema Biteko
Ameendelea
kusema kuwa watanzania wengi wana matarajio makubwa kwenye Sekta ya
Madini na kuongeza kuwa Wizara ya Madini imejipanga katika kuhakikisha
Sekta ya Madini inaendelea kukua kwa kasi huku ikiwa na mchango mkubwa
kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
"Nataka
mfahamu kuwa kama Wizara ya Madini tunapimwa kwa ukuaji wa Sekta ya
Madini, hivyo ni vyema mkahakikisha mnafanya kazi kwa kasi na ubunifu
ikiwa ni pamoja na kujiamini", amesema Waziri Biteko.
No comments:
Post a Comment