HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 16, 2021

MAJALIWA: WATENDAJI JIEPUSHENI NA RUSHWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wajiepushe na vitendo vya kuomba rushwa na urasimu usiokuwa wa lazima katika kuwahudumia wawekezaji ili kujenga imani baina ya sekta binafsi na sekta ya umma

 

Pia, Waziri Mkuu amezitaka Wizara na taasisi zote zinazohudumia wawekezaji kuhakikisha wanawezesha wawekezaji katika maeneo yao kwa kutoa huduma na taarifa muhimu kwa wakati.

 

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Aprili 16, 2021) wakati akihitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa 2021/2022 mwaka wa Fedha 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.

 

Waziri Mkuu amesema tarehe 6 Aprili 2021, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Tanzania akiwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa baadhi ya Taasisi za Serikali alisisitiza masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji na vibali vya kazi.

 

“Mheshimiwa Rais aliielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuimarisha huduma za pamoja (One Stop Centre), kushughulikia malalamiko kuhusu kodi, kuondoa vikwazo katika uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji kupitia mazungumzo, ushawishi, kudhibiti rushwa na kuondoa urasimu kwenye maombi ya vibali vya kazi”.

 

Amesema maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais yenye kujali maslahi mapana ya nchi hii yalikwenda sambamba na uamuzi wake wa tarehe 31 Machi 2021 wa kuunda rasmi Wizara ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuhakikisha kuwa Wizara hiyo inasimamia kikamilifu masuala ya uwekezaji.

 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kueleza hatua mbalimbali za utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia kuhusu Wizara ya Uwekezaji ambazo tayari zimechukuliwa kuwa ni pamoja na pamoja na kuandaa Muundo wa Wizara ambao utaainisha majukumu na mgawanyo wa Idara na Taasisi zitakazokuwa chini ya uwekezaji.

 

“Hatua ya pili ni kupitia Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 ili kubainisha maeneo yenye kuhitaji maboresho ambapo tayari tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 imekamilika na kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ili kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya uwekezaji nchini”.

 

Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa hatua hizo kutaiwezesha Serikali kushiriki kikamilifu katika mikutano na majadiliano ya jumuiya za kikanda yanayohusu masuala ya uwekezaji ikiwemo maandalizi ya Sera ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Pia, Waziri Mkuu ameongeza kuwa hatua hizo zitaiwezesha Serikali kushiriki katika utungaji wa Sera za Uwekezaji kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Itifaki ya Uwekezaji ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika.

 

Kujenga  mazingira rafiki ya uwekezaji na uchumi shindani nchini kwa kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wawekezaji (Online Investors Feedback Platform)”.

 

Kutatua changamoto za wafanyabiashara kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kwa kuratibu majadiliano ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, kutoa elimu na hamasa kuhusu huduma zitolewazo kwenye Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre-OSFC).”

 

Amesema kupitia hatua hizo, Serikali itaweza kuimarisha mifumo ya usajili wa miradi na kutoa Cheti cha Vivutio (Certificate of Incentives), kuunganisha mifumo inayotumika TIC na makao makuu ya Taasisi na kuboresha mfumo wa kuchakata rufaa za vibali vya kazi na ukaazi kwa njia ya mtandao.

 

“Nitumie fursa hii tena kuwakumbusha watendaji wenzangu wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kuhakikisha kuwa muundo na mifumo ya masuala ya uwekezaji inakamilika ndani ya muda ulioelekezwa na Mheshimiwa Rais”.

No comments:

Post a Comment

Pages