HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 12, 2021

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR ATOA ONYO KALI KWA ASKARI WANAONYANYASA WANANNCHI


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za Mandeleo na kufahamu changamoto zinazowasumbuwa Wananchi ndani ya Wilaya ya Magharibi A akimalizia ziara yake ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi kuzitembelea Wilaya zake.

 

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimwa Hemed Suleiman ametoa onyo kali kwa baadhi ya askari wa Vyombo vya Dola wenye tabia ya kuwanyanyasa Wananchi kwa sababu ya ushawishi wa Migogoro ya Ardhi kuacha mara Moja vitendo hivyo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alitoa onyo hilo baada ya kusikiliza  malalamiko ya pande zote mbili yanayohusisha Mgogoro wa Ardhi ambao kwa sasa uko mahakamani  uliohusisha Wakulima na msimamizi wa Shamba liliopo Dole Bibi Shadya Ahmed Abdulla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikuwa katika ziara ya kukagua shuguli za Mandeleo na kufahamu changamoto zinazowasumbuwa Wananchi ndani ya Wilaya ya Magharibi A akimalizia ziara yake ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi kuzitembelea Wilaya zake.

Akizinasihi pande zote mbili kuendelea  kuwa na subra kipindi hichi ambacho tatizo lao liko Mahakamani alikemea tabia ya baadhi ya Viongozi na Watu kutumia migogoro ya Ardhi kuwanyanyasa wenzao na kutahadharisha wazi kwamba Askari ye yote atakayehusika na vitendo hivyo Serikali haitasita kumuwajibisha na hata kumfukuza kazi mara Moja.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwataka wahusika wa Mgogoro huo kusubiri maamuzi ya Mahakama yanayotarajiwa kutolewa ndani ya Mwezi huu ili Yule mwenye haki aweze kupatiwa fursa yake stahiki ambae atastahiki kuendelea kuheshimu upande mwengine.

Alibainisha kwamba si vyema Mizozo ikasababisha Migogoro na hatimae kuleta madhara ambayo inaweza kuondosha Amani inayostahika kudumishwa wakati wote wa maisha ya kawaida.

Akizungumzia Sekta ya Afya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman aliwahakikishia Wananchi wa Shehia ya Mbuzini kwamba Serikali Kuu kupitia Wizara ya Afya na Serikali ya Mkoa wa Wilaya itajikita katika kuona huduma za Afya ndani ya Shehia hizo zinapatikana katika kipindi kifupi.

Alitoa Mwezi  Mmoja na kuuagiza Uongozi wa  Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Uongozi wa Ofisi ya Mkoa Mjini Magharibi na Wilaya ya Magharibi kufanya utafiti utakaosaidia kuona  upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Wananchi wa Shehia ya Mbuzi unatekelezwa ndani ya kipindi kifupi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema haipendezi hata kidogo kuona Wananchi wanafikia hatua ya kuanzisha Miradi ya Ujenzi wa Vituo vya Afya kwa ajili ya kuondosha changamoto zinazowakabili hasa akina Mama Wajawazito lakini hujitokeza baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma kuwa na tabia ya kukwamisha  Miradi hiyo kwa utashi wao binafsi.

Akigusia uharibifu wa mazingira uliopelekea Serikali kuziondosha Familia Tano katika eneo hatarishi liliopo Mtoni Kidatu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uamuzi waliyochukuwa na Viongozi wa Wilaya haukufanya makosa badi ulilenga kunusuru maisha ya Watu hao.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejiridhisha na maamuzi ya Uongozi wa Wilaya na Mkoa kwa kuzihamisha  Familia hizo, vyenginevyo kuendelea kuwaruhusu kuishi eneo hilo hatarishi kunaweza kuhatarisha Maisha yao na matokeo yake Serikali ndio itakayobeba dhima ya matukio ya ajali.

Mheshimiwa Hemed Suleiman amewahakikishia Wananchi hao wa Familia Tano kwamba kikao watakachokutana nao kujadili suala hilo kina lengo la kuona namna gani Serikali Kuu inaweza kusaidia njia zitakazoonyesha muelekeo kwa Familia hizo kuendelea na maisha yao bila ya wasi wasi.

Katika ziara hiyo ya Wilaya ya Magharibi A Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea Wakulima wa Bonde la Bumbwisudi, eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko hapo Chuini Kwanyanya pamoja na Wajasiri Amali wanaojishughulisha na Ukaushaji wa Dagaa hapo Ngalawa.

Wakielezea changamoto zinazowakabili Wakulima, Wananchi na Wajasiri Amali hao walimueleza Mheshimiwa Hemed kwamba baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma wamekuwa kikwazo katika utatuzi wa changamoto zao kiasi kwamba baadhi zimeshafikia zaidi ya Miaka Mitatu sasa.

Akifafanua baadhi ya changamoto hizo Mheshimiwa Hemed Suleiman alitahadharisha wazi kwamba Mtendaji ye yote atakayebainika kuzorotesha maslahi ya Wananchi walio wengi kwa sasa anapaswa kutafuta kazi nyengine ya kufanya kwa vile ile aliyopewa kuhudumia Wananchi itakuwa imemshinda.

Alisema yeye akiwa Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali ataendelea kufuatilia changamoto zote zinazowakwaza Wananchi na Mtendaji atakayebainika  kusababisha uzembe wowote atalazimika kuwekwa pembeni.

Mapema akitoa Taarifa za Serikali Wilaya ya Magharibi A ndani ya kipindi cha Miezi Mitatu hapo Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi A uliopo Kianga Bibi Suzan Peter Kunambi  alisema yapo Maendeleo ya Wastani yalioyopatikana katika Sekta za Kijamii na hata zile za Kiuchumi.

Hata hivyo Bibi Suzan alisema zipo changamoto ya upatikanaji wa huduma ya Maji Safi na salama, Miundombinu ya Bara bara za ndani pamoja na Umeme kwa baadhi  maeneo ndani ya Wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages