Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akitoa salamu za Eid katika Baraza la Eid lililofanyika Msikiti wa Kata ya Mandewa mkoani hapa juzi. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Bakwata Mkoa wa Singida, Jumanne Nkii, Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida, Burhan Mlau na Sheikh wa Msikiti wa Kata ya Mandewa, Salumu Chima
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro amesema anatarajia kuwasilisha katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ajenda ya nia ya Waislamu wa Mkoa wa Singida kutaka kujenga hospitali yao.
Sheikh Nassoro ameyasema hayo wakati akitoa salamu za Eid katika Baraza la Eid lililofanyika Msikiti wa Kata ya Mandewa mkoani hapa jana.
" Taasisi zote zilizopo Tanzania hakuna taasisi yenye rasilimali watu kama Taasisi ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Bakwata ambayo ina majority ya watu tatizo ni watu hao wanatumiwaje nasema Waislamu Mkoa wa Singida tunaweza kuanza kujenga Hospitali yetu ili dada zetu na mama zetu waweze kupata staha." alisema Nassoro.
Nassoro alisema jambo hilo analitanguliza na anatarajia kuliwasilisha kwenye mkutano huo na kuwa hiyo ni ajenda ya waislamu wa mkoa huo na mara moja kamati zitaundwa ili kuanza taratibu za kazi hiyo.
Alisema ana uhakika kazi hiyo itakapo anza watu wa chini, watu wanyonge na taasisi kubwa na matajiri watawaungwa mkono na hospitali hiyo itasimama kama uyoga na watu watashangaa.
Sheik Nassoro alisema walipotoka ni mbali na wanapokwenda ni karibu na kuwa kwa sasa majukumu pia yameongezeka na ni mengi na makubwa hivyo ni wakati wa kujifunga mkanda na muda wa kufanya majungu, fitina na kuwa fulani hafai sasa basi
kwani ni muda wa kusikiliza rai kutoka kwa mtu anayetaka waislamu wa Mkoa wa Singida kupata maendeleo na kuwa ofisi ya Bakwata mkoa ipo wazi wakati wote na kama mtu atakuwa na rai waambiwe viongozi au Katibu ambaye ataiwasilisha.
Alisema kukamilika kwa hospitali hiyo kutatoa ajira kwa mabinti na vijana wa kiislamu ambao ni wauguzi na madaktari ambapo aliwataka waanze mbio za kuyatekeleza hayo kwani wamechelewa mno.
Aidha Nassoro alihimiza kufanyike mara moja hatua za usajili wa Chuo cha Nnujumu ili kipate usajili kama anavyokiangalia kwa umuhimu wake Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery.
Katika hatua nyingine Nassoro alisema muda huu anaokaimu nafasi hiyo kwa udogo wa mambo amejifunza kuwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) linauchache wa wataalamu licha ya kuwepo wataalamu wengi lakini hawapo ndani ya baraza hilo hivyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wataalamu wa sekta zote waingie ndani ya Bakwata ili uislamu upate faida ya taaluma zao.
Nassoro alisema ndani ya Bakwata kuna changamoto ya mambo ya utawala 'Admistration' na kuwa anauhakika ndani ya uislamu kuna wataalamu wa jambo hilo hivyo wasikae nyuma tu kwa sababu wao sio wajumbe wa Bakwata ambapo aliwataka waende ili baraza hilo liwe na sura ya hali waliyonayo na hali ya dunia inavyokwenda.
Nassoro pia alizungumzia changamoto ya ofisi ya Katibu wa Bakwata Mkoa kuwa inapaswa kuboreshwa na kuwa na vitendea kazi kama kopyuta ili viweze kumrahisishia kazi badala ya kwenda kuchapa barua za ofisi kwenye maeneo nje na hivyo kutokuwa na siri ya mambo yao.
" Ni vema kila ofisi zetu kuanzia ngazi ya kata wilaya hadi mkoa zikawa na mfumo wa kompyuta na kuwa na wataalamu wakutengeneza hizo barua ambao ni mabinti zetu wasio na ajira na watakuwa wasiri kwa mambo yatakayokuwa yameandikwa ndani ya barua hizo." alisema Nassoro.
Mwenyekiti wa Bakwata Mkoa wa Singida, Jumanne Nkii alisema uongozi wa Mufti umenyooka lakini changamoto kubwa ipo kwa viongozi wa chini ambao wanaendesha dini yao kwa mazoea hawafuati miongozo ya qulaan, suna na katiba ya baraza kwani baadhi yao wamekuwa wakikurupuka na kujikuta wakiharibu kwa sababu ya tamaa zao.
"Sisi viongozi na waislamu wote kwa ujumla ni vizuri tuendeshe masuala yetu kwa kufuata kauli mbiu ya Mufti wetu isemayo Jitambue, Badilika Acha Mazoea." alisema Nkii.
Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida, Burhan Mlau aliipongeza Kata ya Mandewa kwa kuandaa baraza la Eid kwani kwa mkoa mzima hakuna walioandaa ila ni kata hiyo tu ambapo alimuomba Mwenyezi Mungu awajaalie.
No comments:
Post a Comment