HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 16, 2021

Mkurugenzi Mtendaji LHRC awafunda vijana Dar na Pwani

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga, akizungumza na vijana alipokuwa akifungua Kongamano la Vijana toka Vyuo Vikuu, Vyuo vya Kati na Sekondari jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na Club inayohamasisha Elimu na Maadili kwa Vijana (EEMC) Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

 

 

MKURUGENZI Mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga amewataka vijana kuwa na malengo katika maisha yao na kuhakikisha wanafanya jitihada za kuyasimamia ili yaweze kutimia. Mkurugenzi huyo ameyasema hayo jana alipokuwa akifungua kongamano la vijana toka vyuo vikuu, vyuo vya kati na sekondari jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na Club inayohamasisha elimu na maadili kwa vijana (EEMC).

Alisema kijana mwenye malengo hana budi kuweka jitihada katika kuyakamilisha na kutokubali kukata tamaa hata kama anakumbana na vikwazo fulani kwenye maisha yake. "Kijana mwenye malengo hana budi kung'ang'ania malengo yake katika kuyakamilisha, usikate tamaa wala kukubali kushindwa kirahisi," alisema Bi. Henga akiwasilisha mada yake kwa vijana hao.

Aliwataka vijana kutumia changamoto wanazokutana nazo kama fursa za mafanikio kuelekea katika malengo yao. Ameongeza kuwa hata yeye katika mafanikio yake amekuwa akitumia vikwazo kama fursa kukamilisha malengo jambo ambalo linawezekana kwa vijana endapo watafanya maandalizi na jitihada kukamilisha malengo yao.

"..Jambo la msingi ni kufanya maandalizi kuelekea kukamilisha malengo yako, tujiandae na tufanye kazi kwa bidii na sisi ambao tunasoma tusome kwa bidii sana hakuja jambo zuri linalokuja kirahisi bila kufanya jitihada wewe binafsi..pia tusikubali kupoteza muda 'keep time'...," alisisitiza Mkurugenzi huyo Mtendaji wa LHRC.

Alisema kijana mwenye malengo anatakiwa kujenga mahusiano mazuri na watu mbalimbali (networking)  jambo ambalo linaweza kumsaidia mbeleni kuelekea kukamilisha malengo yake, hivyo kuwataka vijana kuto puuza mahusiano mazuri na watu.

Pamoja na hayo aliwataka vijana kuwa waadilifu na wacha Mungu katika kila jambo wanalolifanya kwani ni moja ya daraja la mafanikio kuelekea kutimiza ndoto zao. Unapokuwa mwadilifu na kumshirikisha Mungu mbele kwa kila jambo lako huwezi kushindwa kamwe, siku zote utafanikiwa katika jambo lako," alisisitiza kiongozi huyo.

Kwa upande wao mmoja wa waratibu wa mkutano huo, David Sospita alisema kongamano hilo kubwa la vijana toka vyuo vikuu, vyuo vya kati na sekondari lililoandaliwa na taasisi ya EEMC toka Dar es Salaam na Pwani na kupewa kauli mbiu ya 'kijana na malengo' limelenga kukutanisha vijana kuwaelimisha na kuchagiza malengo yao.

Alisema limeandaliwa ili kuchochea hamasa ya elimu, elimu dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, elimu ya kujitegemea kwa vijana na pamoja na uongozi na maadili kwa vijana. Aliongeza katika kongamano hilo  linalofanyika Chuo Kikuu cha Muhimbili Dar es Salaam vijana watanolewa namna ya kujiajiri na kutimiza ndoto za malengo yao.

No comments:

Post a Comment

Pages