Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Hakiza binadamu Tanzania (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa.
Waandishi wa habari wa Mtandaoni Vyombo tofauti tofauti wakiwa kwenye mafunzo Morogoro.
NA HAMIDA RAMADHANI, MOROGORO
MRATIBU wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzanaia (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema, wandishi wa habari wa mtandaoni, wanatakiwa kupewa mafunzo ya mara kwa mara kwani eneo hilo limeonekana likikuwa kwa kasi kubwa.
Amesema lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mtandaoni ni pamoja na maono yanayoonekana kukuwa kwa kasi kubwa kwa vyombo vya habari vya mtandaoni siku hadi siku.
Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mtandaoni, leo Jumatatu, tarehe 10 Mei 2021, Mkoani Morogoro, Ole Ngurumwa ambaye kitaaluma ni wakili amesema, vyombo vya habari vya mtandaoni vimepewa sheria ambazo ni kandamizi.
“Kutokana na uwepo wa sheria mbalimbali kandamizi kwa eneo la usimamizi wa vyombo vya habari, Sisi kama watetezi wa haki za binadamu Tanzania tumefungua kesi mahakamani ya kuzipinga sheria hizo,” amesema
Na kuongeza kusema, “Tunaimani mwisho wa mafunzo hayo ya siku tatu, yatawafanya waandishi wa habari wa mitandoni kuwa na uelewa mpana wa masuala mbalimbali ili waweze kutimiza majukumu yao kwa weledi,’’ amesema Ole Ngurumwa.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, akizungumza katika semina hiyo amesema, kumekuwepo na sintofahamu kubwa juu ya kufunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyo fungwa.
“Tunamuomba Rais waawamu ya sita wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aziondoe sheria hizi kandamizi kwa vyombo vya habari,“ amesema Mukajanga.
Akizungumzia agizo la Rais Samia, alilolitoa hivi karibuni la kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa kutokana na sababu mbalimbali amesema, agizo la Rais Samia sio suluhu ya changamoto ya vyombo vya habari kufungiwa na kuminywa visifanye kazi zake kwa uhuru, bali inatakiwa sheria zibadilishwe ili uhuru wa vyombo vya habari uenziwe na viongozi watakaofuata.
"Rais Samia akiapisha makatibu wakuu, aliongelea kidogo suala la uhuru wa habari na aliagiza vyombo vifunguliwe. Hili lina mjadala sababu wengine tulisikia ametamka vyombo vya habari lakini wasaidizi wake wamesema agizo lilihusu vyombo ya habari vya mtandaoni.”
“Kwa sababu ofisi yake haijatoa kauli juu ya tarifa ya wasaidizi wake hao, agizo la kufunguliwa mtandaoni bila shaka hilo ndio sahihi," amesema Mukajanga
Katibu mtendaji huyo amesema “tunadhani bila kushughulikia sheria zinazoongoza, zinazosimamia na kudhibiti kazi zetu, tatizo halitaweza kuondoka.”
“Kwa nia njema hiyo, anaweza akaamua kama hivyo mfungulieni fulani, lakini kama sheria ipo maana yake kesho anaweza pata tatizo mtu mwingine au yuleyule aliyefunguliwa akapata tatizo kutokana na sheria zile zile," amesema Mukajanga.
Amesema, “hii inatupeleka wapi, tunadhani hii inaonesha umuhimu kutazama mazingira yetu kwa umuhimu zaidi."
Naye , Mwenyekiti wa Chama cha Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo amesema, “hakuna safari isiyokuwa na mwisho, tumekuwa katika maumivu kwa kipindi kirefu na kundi la ‘social media’ lilisaidia sana, katika kuhabarisha umma.”
Amesema, wakati kukiwa na mtanziko kwenye vyombo vya habari vingine, mitandao ya kijamii ilifanikiwa kwa sehemu kubwa kuhabarisha kwani wahusika waliokuwa wakihabarisha, haikuwalazimu kuwa sehemu moja.
“Kuna sheria na kanuni mbalimbali zinatukwaza katika utendaji kazi, wakati tukiendelea kupambana kuhakikisha zinaondoka, tuendelee kufanya kazi tukijua kabisa kuna hizi sheria,” amesema Nsokolo
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, (TEF) Deodatus Balile amesema, mchakato wa mabadiliko ya sheria za mtandaoni umeanza kufanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuwaomba wadau kujitokeza kutoa maoni
Amesema, kauli ya Rais Samia haikusema vyombo vya habari vya mtandaoni, “alisema vyombo vya habari vilivyofungiwa, vifunguliwe” na akagusia suala la kanuni ziwe wazi.
Balile amesema, mkanganyiko ulikuja kwa watendaji wa Rais Samia wamekuwa waking’ang’ana ni vya mtandaoni pekee jambo ambalo linaendeleza mjadala wa agizo hilo la Rais.
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya sheria amesema tayari umeanza na kuvitaka Vyombo vya habari vya mtandaoni kushiriki kwani TCRA imeanza, wakatoe mawazo na maoni yao
Na kuwataka waandishi wa habari kuonyesha weledi katika kuhabarisha umma.
Jumanne ya tarehe 6 Aprili 2021, Rais Samia alitoa amri ya kuachia huru vyombo vyote vya habari wakati akihutubia baada ya kuwaapisha makatibu, manaibu katibu wakuu na viongozi wa taasisi za umma, Ikulu ya Dar es Salaam.
Rais Samia alisema, wizara ya habari inapaswa kusimamia vyombo vya habari "nasikia kuna vijivyombo vya habari mmevifungia fungia, sijui viji- TV vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya serikali."
"Vifungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa vyombo vya habari, lakini mhakikishe kila mliyempa ruhusu ya kuendesha chombo cha serikali anafuata sheria za serikali na kanuni ziwe wazi, kosa hili adhabu yake ni hii na mnakwenda kwa adhabu mlizoziweka kwenye kanuni," amesema
Katika kusisitiza hilo, Rais Samia alisema "tusifungie tu kibabe. Wafungulieni lakini tuhakikishe wanafuata kanuni na miongozo ya serikali."
Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari vilivyofungiwa, futiwa leseni au kunyimwa leseni za uendeshaji ni MwanaHALISI, Mawio, Tanzania Daima, Mseto na televisheni ya mtandaoni ya Kwanza TV.
Amesema, mwisho wa mafunzo hayo ya siku tatu, yatawafanya waandishi wa habari wa mitandoni kuwa na uelewa mpana wa masuala mbalimbali ili waweze kutimiza majukumu yao kwa weledi.
No comments:
Post a Comment