HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 10, 2021

SINGIDA AZITAKA HALMASHAURI KUSIMAMIA VYANZO VYA MAPATO


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba jana, wakati akikagua jengo la maabara ya Hospitali ya wilaya iliyopo Old Kiomboi katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo.
Baadhi ya watumishi wa Wilaya ya Iramba wakiwa kwenye kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na  Mjasiriamali  alipotembelea Mnada wa Igumo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na watendaji wa wilaya hiyo  alipotembelea Mnada wa Igumo. Kulia ni Askari Polisi wakiimarisha ulinzi eneo hilo. Katikati ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni.
 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewataka watendaji wa halmashauri kusimamia ipasavyo vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye maeneo yao.

Mahenge alitoa agizo hilo jana wilayani Iramba mkoani hapa katika muendelezo wa ziara zake za kutembelea halmashauri zote kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi, watendaji na wananchi.

Alisema anataka viongozi hao hasa watendaji kujua kuwa kupata mapato makubwa sio lazima kuwa na vyanzo vikubwa kama madini na miradi ya mashamba bali ni  hivihivi vidogo vilivyopo ambapo vikisimamiwa vizuri vitazifanya  halmashauri kupata mapato yakutosha.

"Nataka watendaji na viongozi wenzangu wajue kwamba mnada ni chanzo kizuri sana cha mapato hivyo kitiliwe maanani, kuna dhana kuwa ili kupata mapato makubwa ni lazima kuwepo na miradi mikubwa na vitu vingine vinavyofanana na hivyo hapana hivi hivi vidogo vikisimamiwa vitafanya mambo makubwa," alisema Mahenge.

Dkt.Mahenge alisema katika ziara yake hiyo wilayani humo aliamua kutembelea mnada ikiwa ni chanzo mojawapo cha mapato ambacho kimsingi kinajumuisha watu wengi sana.

Aliyata makundi hayo ya watu kuwa ni wachoma nyama, wauza nguo,mifugo na makundi mengine na kuwa alichojifunza ni kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato licha ya kuwepo kwa makundi hayo.

" Nimejifunza hatuna usimamizi mzuri na kuwa chanzo hicho  kipokipo tu kwa sababu hayupo mtu anaye hakiki upatikanaji wa mapato kama yamepanda au kushuka na kwanini makusanyo yana kuwa yale yale kila wakati.

Alisema katika minada aliyoitembelea amebaini kutokuwepo kwa utaratibu wa kuwa sajili wanunuzi wa mifugo kwenye eneo moja badala yake kila mtu anafanya kivyake jambo linalosababisha upotevu wa mapato.

Dkt. Mahenge alisema kukosekana kwa usimamizi mzuri wa mapato katika maeneo hayo kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa serikali ambao sio waaminifu ambao wamechangia kutotumika kwa maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za ununuzi na uuzaji wa mifugo na badala yake kwa kushirikiana na wanunuzi hao wamekuwa wakifanyia shughuli hizo nje ya maeneo hayo.

Aidha alisema jambo kubwa analolihitaji ni usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato kwenye mifugo na kwa wafanyabiashara wengine ambao wanafanya shughuli za kibiashara kwenye eneo hilo la mnada ambao wengi wao hawana vitambulisho vya ujasiriamali hivyo ametaka kuongezwa kasi ya utoaji wa vitambulisho hivyo kwani wananchi wako tayari lakini hawajapa fursa ya kuvipata. 

Alizitaka timu za ukusanyaji wa mapato za halmashauri kunapokuwa na minada kwenda kujionea ukusanyaji wa mapato badala ya kumuachia mtu mmoja ambaye anaweza kurubuniwa na kusababisha upotevu wa mapato. 

Dkt.Mahenge katika ziara yake alitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la maabara hospitali ya wilaya ambapo hakuridhishwa na gharama halisi zilizotumika kwa ujenzi huu kuanzia msingi hadi hatua ya linta na kumwagiza mkuu wa wilaya hiyo kufanya uchunguzi.

Aidha alikagua ukusanyaji wa mapato katika Mnada wa Igumo na mradi wa maji uliopo Kijiji cha Kyalosangi.

No comments:

Post a Comment

Pages