Mratibu wa mbio za Uhuru (Uhuru Marathon 2021), Innocent Melleck, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 18 wakati wa kutangaza mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2021. Kutoka kushoto ni Mratibu Mwamasishaji Washirika wa Uhuru Marathon, Magdalena Gisse, Mshauri wa Ufundi wa Uhuru Marathon, Suleiman Nyambui na Mratibu wa Mbio, Revocatus Rugumila.
Mshauri wa Ufundi wa Mbio za Uhuru Marathon, Suleiman Nyambui, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa kutambulisha mbio za hizo.
Mratibu Mwamasishaji washirika wa Uhuru Marathon, Magdalena Gisse, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Uhuru Marathon 2021 na kutoa wito kwa kampuni mbalimbali kujitokeza katika kudhamini mbio hizo.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria uzinduzi huo.
Na Mwandishi Wetu
MBIO za Uhuru
Marathon 2021 zinatarajiwa kufanyika Desemba 9, 2021 siku ya kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika katika viwanja vya Leaders Club.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 18, 2021 Mratibu wa mbio hizo, Innocent Melleck, amesema fedha zitakazopatikana katika mbio hizo zitakwenda kuanzisha kituo cha michezo cha Tanzania Uhuru High Perfomance Centre.
"“Kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2021-2024 tuwe tumepata fedha za kununua na kujenga kituo cha michezo ambacho kitatumika kama sehemu ya kuibua, kukuza na kuwajenga wanamichezo hasa riadha uwezo wa kuwa washindani wakubwa katika mchezo wa riadha ndani na nje ya nchi yetu.”alisema Melleck.
Aliongeza kuwa Kituo hicho kinatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh. Bilioni 4 ambapo kitakuwa na wakufunzi waliobobea katika fani za mchezo wa riadha kitaifa na kimataifa na kitajulikana kwa jina la Tanzania Uhuru High Perfomance Centre.
“Katika hili tutaomba pia serikali itazame kwa jicho la pili umuhimu wa kutenga ruzuku kidogo kwa ajili ya kufanikisha jambo hili muhimu kwa historia ya Taifa letu.”
Naye Mratibu Mwamasishaji Washirika wa Uhuru Marathon, Magdalena Gisse, ametoa rai kwa mashirika yote sio tu kutoa michango au kufanya udhamini bali pia kushiriki katika mbio hizi.
“Sisi ni wakimbiaji wazuri sana na tunamatumaini kwamba hii itakuwa nafasi yetu kuonesha mataifa mengine kwamba watanzania tunaweza kwa sababu hii ndio marathon ya kwanza inasherehekea Uhuru wake.
“Mtu yeyote ambaye mbio hizi zinamgusa au anapenda michezo, anapenda kuona watanzania tunajitangaza vizuri na kuweza kufika mbali kimichezo basi hii ndio itakuwa nafasi yake ndio maana tumesema tunaruhusu hadi wadhamini binafsi waje kudhamini mbio hizi.” Alisema Gisse.
Mshauri wa Ufundi wa Mbio za Uhuru Marathon 2021, Suleiman Nyambui, amesema ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa kituo cha michezo cha Tanzania Uhuru High Perfomance Centre watu wengi wanatakiwa wajisajili katika mbio hizo, watu na kampuni watoe udhamini kwa wingi.
Aidha nyambui amewataka wazazi kuwasajili watoto wao kushiriki nao katika mbio za kilometa 2.5 kwa ajili ya watoto ambazo zitawajengea watoto kupenda michezo wakiwa wangali wadogo.
Mwaka huu mbio zitakuwa kilometa 42 Wanawake na wanaume km 21 wanaume na wanawake, km 10 wanawake na wanaume km 5 wanawake na wanaume km 3 (Mbio maalum za viongozi) km 2.5 mbio za Watoto.
No comments:
Post a Comment