Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Joseph Haule akikagua na kutoa maelekezo kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Eliseus Mtenga kufanya matengenezo na kusafisha miundombinu ya barabara, mifereji na madaraja mkoani hapo.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Eliseus Mtenga, akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), ambao walikuwa wanakagua miundombinu ya barabara katika eneo la Nyaishozi Kinondoni mkoani humo.
Na Mwandishi Wetu
WAKALA ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam wameagizwa kufanya matengenezo na kusafisha barabara, mifereji na mafumo ya kupitisha maji ya mvua ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Maagizo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), James Haule wakati wa ukaguzi wa barabara katika eneo la Masana, Nyaishozi, Dawasa na Daraja la Mapinga.
Mwenyekiti huyo alisema ziara yao imegundua kuwa TANROADS mkoa imeshindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo hali ambayo inachangia uharibifu kwenye barabara na mifereji.
Haule alisema wameshuhudia takataka zimejaa katika mifereji iliyopo Masana, Nyaishozi na Dawasa ambapo wao wametoa hela za matengenezo hali ambayo inasababisha barabara kuharibika.
Alisema pia wamegundua kuwepo baadhi ya wananchi kuelekeza maji machafu katika mifereji na makalavati hali ambayo inachangia mifereji kuzima hivyo TANROADS mkoa inawajibu wa kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa masafi ili barabara ziwe salama.
“Ziara hii imebaini mapungufu mengi hasa mifereji ya kupitisha maji kuziba, lakini maeneo mengine hakuna mifereji haina muendelezo kupitisha maji kwenda katika eneo la mwisho jambo ambalo tumewaagiza TANROADS watatue tatizo hilo mapema,” alisema.
Aidha, akizungumzia changamoto ya daraja la Mpiji ambalo ni mpaka wa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani amemtaka mkandarasi aongeze kati ili kazi iweze kukamilika kwa wakati.
Mwenyekiti huyo alisema matarajio yao ni kuona changamoto hiyo ya kuharibu daraja inatatulika kama TANROADS ilivyosema jambo ambalo litahakikishia daraja hilo linakuwa salama zaidi.
Haule alisema iwapo maji yataachiwa yaendelee kutuama yatachangia barabara kuharibika na kutokudumu kwa muda mrefu hali ambayo itaigharimu Serikali kutoa fedha nyingi na kusababisha maeneo mengine ya nchi yanabaki nyuma.
Aidha, Haule amezitaka mamlaka za jiji, manispaa na halmashauri kushirikiana na TANROADS na Wakala ya Barabara Mijini na Vijiji (Tarura) kuhakikisha wanafanya kazi za kusafisha barabara hawapi takataka kwenye mifereji.
Kwa upande wake Meneja wa RFB, Eliud Nyauhenga ameziagiza mameneja wa TANROADS na Tarura nchini kote kufanya matengenezo ya barabara na kuondoa takataka kwenye mifereji kabla ya mvua za vuli hazijaanza.
Nyauhenga alisema iwapo matengenezo ya barabara na usafi wa mifereji yatafanyika kila mara ni wazi miumbombunu itadumu kwa muda mrefu.
“Mwaka wa jana RFB imetoa zaidi ya Sh. bilioni 900 ambazo zimefanya matengenezo ya barabara, daraja na mifereji na mwaka huu tutaendelea kutoa ili miundombinu yetu iwe salama,” alisema.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Eliseus Mtenga, alisema wamepokea maelekezo ya bodi hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa wakati.
Mtenga alisema wamejipanga kabla ya mvua kuanza kunyesha kufanyia matengenezo na kusafisha mitaro yote ambayo imejaa takataka.
“TANROADS imejipanga kutunza na kuendeleza miundombinu ya barabara hapa mkoani, hizi changamoto zilizobainika tutazitatua kwa haraka kama tulivyoelekezwa,” alisema.
Akizungumzia matengenezo ya gati la kuzuia uharibifu wa Daraja la Mpiji alisema yapo katika hatua za mwisho na kwamba katikati ya mwezi Septemba mkandarasi atakabidhi.
“Hapa tunajenga magabioni ambayo yataweza kuzuia mmomonyoko wa daraja hili la mpiji ambalo ujenzi wake umegharimu Sh. milioni 296,” alisema.
No comments:
Post a Comment