Afisa Usimamizi wa Kodi Mkoa wa Kagera, Alex Mwambenja, akizungumza na waandishi wa habari baada ya semina ya wafanyabiashara .
Na Lydia Lugakila, Bukoba
Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Kagera imewataka wafanyabiasha katika Manispaa ya Bukoba kuhakikisha wanakuwa na namba ya utambulisho kwa mlipa kodi (TIN) ili kukwepa adhabu ya shilingi milioni moja na laki 5 kwa wasiokuwa nayo.
Kauli hiyo imetolewa na afisa usimamizi wa kodi ambaye pia anasimamia elimu na huduma kwa mlipa kodi Mkoani Kagera Alex Mwambenja katika semina ya wafanyabiashara iliyolenga kuwajulisha mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi yaliyotokea mwaka 2021 iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Bukoba.
Mwambenja amesema kuwa kila mfanyakazi ni lazima awe na TIN-yaani namba ya utambulisho kwa mlipa kodi na kuwa kukosa kuwa na namba hiyo wakati ukiwa katika shughuli za kiuchumi adhabu yake au faini ni kulipa shilingi milioni moja na laki 5 huku wanaokahidi kupelekwa mahakamani.
"TIN ni bure mfanyabiashara ndiye mlipa kodi hivyo kila mfanyakazi anatakiwa awe na TIN na ukichelewa kuipata ndani ya siku 15 baada ya shughuli za biashara T.R.A inapaswa kukutoza kiasi hicho cha fedha na ikifika miezi 6 huna TIN kabisa haijalishi udogo au ukubwa wa biashara yako hilo ni kosa adhabu yake utatakiwa uilipe papo hapo wala si kwa awamu" alisema Afisa huyo.
Akitoa ufafanuzi wa namna ya kupata TIN hiyo amesema mfanyabiashara mlipa kodi atatakiwa afike katika ofisi za mamlaka hiyo akiwa na nakala ya kitambulisho cha serikali, kitambulisho cha mpiga kura, passport ya kusafiria kitambulisho cha taifa au akikosa baadhi ya nakala hizo basi awe na barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.
Aidha Mwambenja ameongeza kuwa zoezi la kusajili walipa kodi wapya kwa sasa lipo Dar es salaam ambapo limechukua nguvu katika mikoa tofauti tofauti kwa kupita duka kwa duka ili kuwasajili walipa kodi hao wapya ambapo mikoa mingine ikiwemo Kagera zoezi hilo litafanyika lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtu anayestahili kulipa kodi aweze kulipa.
Amesema zoezi hilo halitafanyika ofisini bali litakuwa mtaa kwa mtaa ambapo wataambatana na mashine zao, wataalam wa kodi, utoaji wa vyeti vya TIN huku wasio na TIN kupatiwa.
Hata hivyo amewaomba wananchi kutoa ushirikiano mara zoezi hilo litakapo anza huku akiwahimiza walipa kodi kuendelea kuchangia kodi kwa hiari na kuepuka kukimbilia mitini badala yake wasjili biashara zao ili kupewa TIN.
No comments:
Post a Comment