Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ibrahim Pazia, akipata chanjo hiyo.
Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Mkalama Hamisi Ramadhani akizungumza kwenye mafunzoh hayo.
Na Dotto Mwaibale, Mkalama
MAFUNZO yaliyotolewa kwa Watoa Huduma wa Afya wilayani Mkalama mkoani Singida kwa ajili ya kutoa elimu dhidi ya Uviko 19 kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na kupokea chanjo yamezaa matunda baada ya baadhi ya wahudumu hao kuelewa na kuchoma chanjo hiyo hivyo kuwa mabalozi wa kwenda kutoa elimu hiyo kwa wananchi.
Mafunzo hayo yalitolewa jana wilayani hapa kutoka kwa timu ya uhamasishaji wa chanjo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Maofisa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo ya chanjo kwa Wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkuu wa wilaya hiyo Sophia Kizigo alisema changamoto ya wananchi kutojitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo hiyo kwa idadi ya watu 10 inaweza kuwa ni moja ya sababu iliyosababisha wilaya hiyo na zingine hapa nchini kuwa na idadi ndogo ya watu walioitikia mwito wa kupata chanjo.
" Utaratibu wa kutoa chanjo hiyo ilikuwa wapatikane watu 10 ili dawa itakayotumika isiweze kuharibika hivyo watoa huduma walikuwa wakisubiri ifike idadi hiyo ndipo watoe chanjo,". alisema Kizigo.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Jamii na Lishe, Dinah Atinda alisema uelewa na uhamasishaji mdogo kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan umechangia kwa kiasi kikubwa watu kutojitokeza kwa wingi kwenda kuchanjwa.
" Serikali imetumia fedha nyingi kuagiza chanjo lakini wananchi bado hawaja kwenda kuchanjwa hivyo imetengeneza mpango mkakati harakishi wa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu chanjo ya Uviko 19 na kuchanja" alisema Atinda.
Alisema hatua iliyofikiwa na Serikali ni kuanza kutoa mafunzo kuanzia ngazi ya Taifa hadi kuwafikia walipo wananchi.
Richard Magodi kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Mpango wa Taifa wa Chanjo alisema baada ya kutokea vifo vingi maeneo mbalimbali duniani kutokana na ugonjwa huo sasa hivi vifo hivyo vimeanza kupungua kutokana na kutumia chanjo.
" Na sisi kama nchi na pia Taifa ambalo lipo miongoni mwa mataifa mengine lilikuwa ni jukumu letu kuishauri Serikali na kuanzisha mpango huu wa chanjo," alisema Magodi.
Magodi alisema chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote baada ya kuhakikiwa na wataalamu na tayari imetolewa nchi mbalimbali duniani.
Wakizungumza baada ya kupata mafunzo hayo Mchungaji Setina Kanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Dumanga alisema sasa anakwenda kuwaeleza waumini wake umuhimu wa kupata chanjo hiyo.
Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Mkalama Hamisi Ramadhani alisema awali alikuwa alielewi zoezi hilo la chanjo kutokana na kuwa na maneno mengi ya kukanganya lakini sasa anakwenda kutoa elimu hiyo kwa wananchi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bosco Charles aliwataka washiriki wote waliopata mafunzo hayo kwenda kuhamasisha wananchi katika maeneo yao ili wapate chanjo hiyo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliopata chanjo hiyo ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ibrahim Pazia, Afisa Elimu Taaluma Sekondari, Ernest Stephen, Kalisti Faustin ambaye ni Muuguzi, Nyandewa Zabron, Afisa Muuguzi Salum Mputa, Farida Seleman, Aizack Zabron.
No comments:
Post a Comment