HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 28, 2021

WANANCHI KATA YA KEREBE WALIA NA BEI YA UMEME

 

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila akizungumzia na wananchi.


Na Lydia Lugakila Muleba

 

Wananchi wa Kata ya Kerebe, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera wameilalamikia kampuni ya JUMEME mbele ya Mkuu wa wilaya kwa kuwauzia umeme kwa bei kubwa, hela inakatwa lakini hawapati namba za umeme (token) walionunua na fedha yao hairudishwi.

Wakitoa malalamiko hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila alipowatembelea kisiwani humo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero zao.

Wananchi hao wamesema umeme umekuwa ni kero kwao pamoja na kutozwa fedha nyingi kununua bado wamekuwa hawapati umeme kwa uhakika.

Mmoja wa wananchi waliotoa kero hiyo  Philibert Kanyambo amemuomba Mhe. Nguvila kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya umeme ambapo wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu bila kupata suluhisho.

Akijibu kero hiyo, Mhe. Nguvila amemtaka mkandarasi JUMEME anayetoa huduma hiyo kuhakikisha ndani ya siku mbili anarudisha hela za wananchi walionunua umeme pasipo kupata namba za umeme (token) na kama hana uwezo wa kutoa huduma hiyo ni vema ajiondoe katika Huduma hiyo ili itafutwe kampuni nyingine yenye uwezo itakayoondoa kero kwa wananchi.

"Hawa wananchi wanahitaji huduma na sio huduma igeuke kero kwao. Nakuagiza ndani ya siku mbili wananchi wote walionunua umeme na hawakupata token warudishiwe hela zao kinyume na hapo nakuchukulia hatua," ameeleza Mhe. Nguvila.

Akijibu malalamiko hayo ya wananchi Meneja Mradi wa kampuni ya umeme ya JUMEME mkoa wa Kagera Ndg. Ahmed Rajabu amekiri kuwa ni kweli kulikuwa na tatizo hilo la kimtandao watu kununua umeme na hawakupata namba (token) ila kwa sasa tatizo hilo limetatuliwa ikiwa ni pamoja na kupunguza bei ya unit moja ya umeme kuwa Tsh.100.

Mbali na kero hiyo wananchi wa kata ya Kerebe wameiomba Serikali kuwajengea mradi wa maji utakaowawezesha kupata maji safi na salama kwani wanatumia maji yasiyotibiwa kutoka ziwani ambayo tayari yamechafuliwa na shughuli za kibinadamu hali ambayo ni hatari kwa afya zao, ujenzi wa ghati la kuvukia pindi wanapopanda na kushuka kwenye boti, Afisa Uvuvi wa Kata ya Kerebe kufuata taratibu na kanuni pindi anapotekeleza majukumu yake na sio kutumia nguvu kuwakomoa watu, Mamlaka ya Bandari TPA kuwatoza kiwango kilicho halali Tsh 22/= kwa kilo na sio zaidi ya hapo na wanaposafiri na samaki wa mboga, mikungu ya ndizi na kuku kwa matumizi ya chakula waondolewe tozo.

Halmashauri kuwapa mikopo itakayowawezesha kujikwamua kimaisha, huduma ya vipimo kwenye zahanati ya Kerebe iboreshwe kwa kuongezewa vipimo zaidi sio vya malaria pekee, ombi la kuwa na kituo cha Polisi ili kuimarisha ulinzi, kuwezeshwa boti ya usafiri itakayowasaidia kipindi wanapopata shida mfano kumpeleka mgonjwa hospitali kwani tayari Mbunge aliwapa mashine na ombi la kuletewa Afisa Kilimo kwaajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu na kutatua migogoro baina ya wafugaji na wakulima.

Kutokana na kero hizo Mhe. Toba amemuagiza kaimu Mkurugenzi Ndg. Charles Ntaki kumfungulia mashtaka ya kinidhamu Afisa Uvuvi wa kata ya Kerebe huku akimtaka amuondoe katika kituo hicho na kumrejesha afanye huduma za ofisini, amewasihi watumishi na viongozi kuwa msaada kwa wananchi na si kutumia ubabe katika kusuluhisha migogoro ya wananchi ni vema wakawaelimisha wananchi kwa utaratibu.

Aidha, Mhe. Nguvila ameitaka Idara ya Maendeleo ya jamii kufika kisiwani Kerebe na kutoa elimu kwa vijana na akina mama ili kuwawezesha kupata mikopo itakayowainua kimaendeleo. Na kuwaeleza kuwa suala la mradi wa maji tayari mchakato wake umeshaanza ambapo wamepatikana wafadhili kutoka Ufaransa watakaofika wakati wowote na kuanza kazi ya usanifu. Na suala la ujenzi wa kituo cha polisi amewaeleza kuwa ni vema wao wakaanzisha mchakato wa ujenzi ili Serikali ije kuwaunga mkono wakiwa wanaendelea na ujenzi huo.

Katika ziara hiyo aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini Mhe. Charles Mwijage (MB) ambae amemshukuru Mhe. Nguvila kwa kufika kisiwa cha Kerebe na kujionea hali halisi ya maisha ya wananchi wa kata ya Kerebe. Huku akiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kueleza kuwa tayari Serikali imetoa Tsh. milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu shule ya msingi Kerebe.

Kwa niaba ya wananchi Diwani wa Kata ya Kerebe, Mhe. Sudi Seif amemshukuru Mkuu wa Wilaya pamoja na wote alioongozana nao katika ziara hiyo ambao ni wajumbe wa Kamati ya Usalama wilaya, Mwakilishi wa Katibu wa Chama cha Mapinduzi, Ndugu. Magesa Kengela ambae pia ni Katibu wa wazazi wilaya, Waheshimiwa Madiwani na wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi ambapo nao walipata nafasi ya kujibu kero mbalimbali kulingana na maeneo yao ya kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages