Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara yake ya kukagua maandalizi ya uzinduzi wa Huduma Pamoja katika Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania, Dar es salaam.
Na Selemani Msuya
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua vituo vya huduma pamoja siku ya Jumatatu Septemba 6 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Ndugulile alisema uzinduzi wa vituo hivyo vya huduma pamoja ni muendelezo Serikali kuimarisha huduma zinazotolewa na Shirika la Posta Tanzania.
Alisema Shirika la Posta lilikuwa limepoteza mwelekeo lakini kwa kipindi cha miezi tisa sasa wamekuwa wakifanya mabadiliko ili liweze kuwa na tija kwa nchi na wananchi.
"Septemba 6 siku ya Jumatatu mwaka huu Waziri Mkuu Majaliwa atazindua vituo vya huduma pamoja ambavyo vitachochea ufanisi wa kutoa huduma mbalimbali ambazo wananchi wanahitaji," alisema.
Waziri Ndugulile alisema vituo vya huduma pamoja ambavyo vitazinduliwa na Waziri Mkuu Majaliwa ni Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhaminia (RITA), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Halmashauri.
Dk.Ngugulile alisema vituo vya huduma pamoja vitasaidia kupunguza foleni ambazo zimekuwa zitokea katika maeneo mengine ya watoa huduma Serikalini.
Waziri huyo alisema kwa kipindi cha miezi tisa pia Shirika la Posta limefanikiwa kutoa huduma za biashara mtandao na posta kiganjani ambazo zimeanza kurejesha heshima ya shirika.
Alisema maboresho hayo yamewezesha shirika hilo kuweza kushirikiana na mashirika ya Posta zaidi 650,000 duniani.
Kwa upande wake Kaimu Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo alisema mikakati yao kwa sasa ni kufikisha vituo vya huduma pamoja katika mikoa 10 ambayo ni Dar es Salaam, Unguja, Chakechake, Morogoro, Tanga, Arusha, Dodoma, Mwanza, Kigoma na Mbeya.
"Hivi vituo vya huduma pamoja tumejipanga kuvitekeleza kwa awamu tatu ambapo hadi Desemba 2025 kila eneo la nchi vitapatikana," alsema.
Alisema uanzishwaji wa huduma hizo mpya umewezesha shirika kuongeza mapato hadi kupata faida zaidi ya Sh.bilioni 3.
Mbodo alisema kupitia huduma ya duka mtandao ambao inasimamiwa na shirika wamefanikiwa kuata zaidi ya Sh.milioni 300.
Halikadhalika alisema huduma ya Posta Kiganjani nayo imekuwa chanjo sahihi cha mapato kwa shirika huku akiwasisitiza Watanzania kutumia huduma hizo.
Kaimu Posta Masta Mkuu huyo alisema lengo na mikakati yao ni kuhakikisha kuwa shirika hilo linakuwa mchangiaji mkubwa wa uchumi wa nchi kama nchi nyingine duniani zinavyofanya.
No comments:
Post a Comment