HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 04, 2021

TCU YATOA MWENENDO WA UDAHILI SHAHADA YA KWANZA MWAKA WA MASOMO 2021/2022

Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 4 kuhusu kufungwa kwa Awamu ya Pili ya Udahili ifikapo Septemba 6, 2021



Dar es Salaam, Tanzania

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inapenda kufahamisha umma na wadau wa Elimu ya Juu nchini kuwa Awamu ya Pili ya Udahili na zoezi la kuthibitisha udahili kwa waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika Awamu ya Kwanza ya Udahili kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2021/2022 litafungwa Jumatatu tarehe 6 Septemba, 2021. 


Profesa Kihampa amesema zoezi litakaloendelea ni vyuo kuchakata na kuidhinisha maombi ya udahili yaliyopokelewa vyuoni katika Awamu ya Pili ya Udahili. 

"Zoezi la kuchakata na kuidhinisha maombi hayo litakapokamilika, majina ya waliodahiliwa katika Awamu ya Pili ya Udahili yatatangazwa na vyuo husika tarehe 18 Septemba, 2021."

Baada ya kukamilika kwa Awamu ya Pili ya Udahili, Awamu ya Tatu ya Udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2021/2022 itaanza rasmi tarehe 18 hadi 24 Septemba, 2021. 

Tume imewataka waombaji ambao bado hawajatuma maombi ya udahili mpaka sasa watumie muda huu uliobaki vizuri kutuma kwa usahihi maombi yao ya udahill kwenye vyuo wanavyovipenda.

Tume inaelekeza Taasisi za Elimu ya Juu nchini kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi. Aidha, waombaji na vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kama inavyoonekana kwenye kalenda ya udahili iliyoko katika tovuti ya TCU (www.tcu.o0.tz).
 

MWENENDO WA UDAHILI

Zoezi la udahili wa Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini linaendelea vizuri. Waombaji wanaendelea kutuma maombi yao katika Awamu ya Pili la Udahili. Wale waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja wanaendelea kujithibitisha kwa kutumia namba Za siri walizotumiwa kwa njia ya ujumbe mfupi au Barua pepe.

 

Mpaka sasa jumla ya waombaji 31,395 waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja, kati ya 35,548 wameshajithibitisha katika chuo kimojawapo. Hivyo, Tume inawahimiza wale ambao bado hawajajithibitisha wakamilishe uthibitisho wao kwa kupitia akaunti zao kwenye vyuo wanavyovipenda. 


Aidha, Tume inapenda kufahamisha umma kuwa waombaji udahili wote wanaoshiriki mafunzo kwa mujibu wa sheria katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutokuwa na hofu kwani muda wa kujithibitisha utaongezwa ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kujithibitisha kabla ya mwaka wa masomo kuanza.

 

KWA WAOMBAJI UDAHILI NA TAASISI ZA ELIMU YA JUU NCHINI

Waombaji udahili wa Shahada ya Kwanza wanakumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika. 

Kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha au kutaka kubadilisha uthibitisho wao, vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa. 

 

Hivyo, wawasiliane na vyuo wanavyotaka kujithibitisha kupitia madawati yao na vyuo vitapokea taarifa zao na kuzifanyia kazi.

Tume inaelekeza Taasisi zote za Elimu ya Juu nchini zinazofanya udahili wa Shahada ya Kwanza kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika zoezi la udahili ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima kwa waombaji udahili na wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages