HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 04, 2021

Nguvu ya Pamoja itatokomeza madawa ya kulevya - Dk. Mkuya



RAYA HAMAD – OMKRM, KOA WA MJINI MAGHARIBI

 

Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji nguvu ya pamoja ili kuhakikisha nchi inashinda vita hio na jamii haina budi kuongeza kasi ya kushirikiana katika kupambana na janga hili na kuwaokoa walioathirika.

 

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt Saaada Mkuya Salum ameyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi mipango sera na utafiti Bi Daima Mohamed Mkalimoto wakati akiyafunga mafunzo ya huduma masafa kwenye ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani.

 

Dkt Saada amesema matatizo yanayofanywa na watumiaji wa dawa za kulevya katika jamii yasipelekee kuwakataa na kuwatenga, kwani wao bado ni sehemu ya jamii yetu.

 

‘Tuendelee kuwafikia zaidi na kuwapatia taaluma juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuwapa ushauri nasaha, kwa namna hii sisi tutakuwa chanzo cha kuwaepusha na msongo wa mawazo, naomba kutoa wito kwetu sote tusimame pamoja katika kuiokoa jamii yetu” alisisitiza Dkt. Saada.

 

Aidha amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaendelea kuchukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto ya matumizi, uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya na madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya.

 

Kumbukumbu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa kuna takriban watumiaji wa dawa za kulevya 10,000 kati yao watu 3,200 wanatumia dawa za kulevya kwa kujidunga sindano, hali inayohatarisha maisha yao na jamii inayowazunguka.

  

Dkt Saada ametoa shukrani kwa Jumuiya ya waliopata nafuu (Recovery Community) kwa uamuzi wao wa kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la utoaji wa elimu kwa jamii juu ya athari ya matumizi ya dawa za kulevya.

 

Kuwafikia walioathirika wa dawa za kulevya na kuwapatia huduma stahiki ambazo zitawasaidia kujiokoa na jinamizi la utumiaji wa dawa za kulevya jambo ambalo linadhihirisha ushiriki wao kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

Mkurugenzi wa huduma masafa ndugu  Abdulrahman Abdallah Mani aliyepata huduma nafuu kutoka kwenye matumizi ya dawa za kulevya na mmoja kati ya waandaaji wa mafunzo hayo amesema kuwa wanampango wa kuanzisha kituo kijulikanacho kama Drop in Centre.

 

Kituo hicho kitawakusanya vijana mara baada ya kutoka katika nyumba za upataji nafuu na kuwasaidia shughuli za kufanya na kujiendeleza ili kuepuka vishawishi vya kurudia tena matumizi ya dawa za kulevya.

 

Mani amesema kituo kitasaidia kutoa fursa mbali mbali kwa walioathirika wa dawa za kulevya na huduma rafiki   ikiwemo elimu, ushauri nasaha kwani wengine hujiingiza pasina kufahamu athari ya janga hili.

 

Nae mkufunzi wa mafunzo hayo Bwana Abdalla Badrus kutoka Mombasa Kenya amesema kuwa taaluma iliyotolewa katika kuwafuatilia vijana walioko kwenye mazingira magumu ya matumizi ya dawa za kulevya hapa Zanzibar itasaidia kujenga nguvu za pamoja katika kuijenga Afrika ya Mashariki isiyo na matumizi ya dawa za kulevya.

 

Badrus amesema iwapo washariki hao watajitahidi kuandika na kuomba miradi kwa kutumia elimu aliyowapatia na mtiririko wa kiuandishi wenye kufuata vigezo hakuna shaka kituo cha Drop in center kitakuwa endelevu na huduma itawafikia vyema walengwa.

 

“hakikisheni mnajituma na kuwa wabunifu mkiandika vizuri wahisani watawaitika misaada itawafikia na mtaweza kutoa huduma kwa kuwafikia vijana walio wengi ambao ndio waathirika wakuu wa matumizi ya dawa za kulevya” alisisitiza Badrus.

 

Mafunzo hayo ya siku 4 yameandaliwa na Jumuiya ya waliopata nafuu (Recovery Community) ambapo washiriki 50 kutoka taasisi za Serikali na Binafsi wameshiriki wakiwemo Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Maafisa wa Chuo cha Mafunzo, Vijana waliopata nafuu na baadhi ya asasi za kiraiya.

No comments:

Post a Comment

Pages