HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 18, 2021

TUTENGENEZE JAMII YENYE IMANI KUEPUKA UVUNJIFU WA AMANI - MAMA ZAINAB


MKE wa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, amewataka wazazi kujikita katika kuwapatia watoto wao elimu ya dini ili kuwajengea mustakbali mwema wa maisha yao duniani na akhera.

Mama Zainab ameyasema hayo leo katika mashindano ya kuhifadhi Qurani, yaliyoandaliwa na Madrasat Swabrul-Imaan ya Mtoni Kidatu wilaya ya Magharib 'A' Unguja na kuzishirikisha madrasa sita.

Amesema vijana watakapojengwa katika imani ya dini na kuhifadhi Qurani katika nyoyo zao, dunia itakuwa sehemu salama kwani watakuwa ni vijana wema wenye kuepuka vitendo viovu katika jamii.
 
"Wazazi tuendelee kushirikiana vyema na walimu wetu ili kuendelea kuuimarisha mustakbali mwema wa watoto wetu" amenasihi Mke huyo wa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Sambamba na hayo amewataka wazazi kuhakikisha wanatoa vipaombele kwa watoto katika elimu zote na badala yake sio kuipa nguvu elimu ya dunia wakasahau ile ya kiimani ya akhera.

Amekumbushia pia uwepo wa vijana wenye elimu ya dini na imani kutapelekea kuzalisha viongozi bora katika familia na Taifa kwa ujumla, kwakusema " Hata kiongozi wa dini yetu ya kiislamu Mtume Muhammad (S.A.W) alitakiwa na Mola wetu kusoma jambo lililomfanya aweze kuitangaza dini ya kiislamu hali ya kuwa ana elimu nayo".

Aidha amewataka waalimu kuendelea kuchukua jitihada zaidi ili watoto hao waweze wakuingia katika mashindano makubwa ikiwemo kuiwakilisha Nchi katika ngazi ya kimataifa.

Naye mlezi wa madrasa hio Dokta Abubakar Makame Hafidh, akimkaribisha mgeni rasmi amesema, maendeleo  makubwa ya wanafunzi na madrasa hio yatapatikana kutokana na jitihada na mashirikiano ya wazazi na waalimu.

Akisoma risala ya madrasa hio yenye wanafunzi takriban 250, mwanafunzi Salama Bakari Ali, amesema moja ya malengo ya madrasa hio ni kuzalisha viongozi bora katika jamii, pamoja na kueleza changamoto zao.

Miongoni mwa changamoto  zilizoainishwa ni pamoja na kukosa tenki la maji ambalo linatoa huduma kwa jamii, ufadhili wa kuwasaidia watoto yatima waliopo katika madrasa hio, kukamilisha matengenezo ya jengo lao la madrasa kwa hatua ya plasta, mazulia kwaajili ya vikalio pamoja na kukosekana kwa zawadi za kuwazawadia washindi yanapotokea mashindano kama haya ya kuhifadhisha Quran, pamoja na kumtaka Mama Zainab kuwasaidia kuwatafutia misaada.
 

No comments:

Post a Comment

Pages