Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (hawapo pichani) wakati akizindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania na baadhi ya Watendaji wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati akizindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Na James Mwanamyoto, Dar es Salaam
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Mhe. Mchengerwa amesema, mafunzo watakayoyapata watumishi hao yatasaidia kuwajenga kimaadili, kutambua na kuiishi miiko ya Utumishi wa Umma, kujua mwelekeo wa Serikali, kuwa na mienendo sahihi inayotakiwa katika Utumishi wa Umma na kuwajengea uzalendo kwa taifa.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa Watumishi wa Umma kuwajenga kiutendaji kwasababu leo hii ukipita kwenye taasisi za umma utabaini baadhi ya Watumishi hawako hai kiutendaji kwa sababu ya kukosa mafunzo elekezi ambayo yangewajengea nidhamu ya utendaji kazi,’’Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, ukosefu wa mafunzo kwa Watumishi wa Umma yanasababisha baadhi ya Watendaji na Watumishi kutoelewana kwasababu binafsi hali inayofanya baadhi ya Watendaji kutowapangia majukumu watumishi walio chini yao hivyo taifa linakosa mchango wao wakati Serikali inawalipa mshahara.
Katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa amewataka Waajiri kuzingatia taratibu za kushughulikia masuala ya nidhamu ili kulinda haki za Watumishi wa Umma.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza na Wajumbe wa Bodi, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Chuo cha Utumishi wa Umma kina jukumu kubwa la kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Umma na kuwaandaa wanaoingia kwenye Utumishi wa Umma ili wawe na mwenendo bora.
Ameongeza kuwa, Chuo hicho hakitakiwi kushindana na vyuo vingine kwasababu hata wahitimu wa vyuo vingine wanapaswa kujengewa uwezo kiutendaji na chuo hicho pindi wanapoingia kwenye Utumishi wa Umma.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Florens Turuka amesema Bodi yake inatambua dhamana kubwa waliyopewa na Serikali katika kuhakikisha Chuo kinatoa mafunzo yatakayojenga Utumishi wa Umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Turuka amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo pamoja na Mhe. Waziri Mchengerwa kwa kuwateua Wajumbe wa Bodi yake ambapo ameahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii, juhudi na weledi ili chuo kitimize majukumu yake kikamilifu.
No comments:
Post a Comment