HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 06, 2021

HESLB yaibuka mshindi tuzo za NBAA 2020

 
Mhasibu Mkuu wa  Serikali CPA(T) Leonard Mkude, akikabidhi tuzo ya mshindi wa tatu kwa taasisi za umma zinazotumia mwongozo wa 'IPSAS' katika uandaaji wa hesabu kwa mwaka 2020 Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) CPA (T) Brown Obeligwe Shimwela. 

Na Mwandishi Wetu


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeibuka mshindi wa tatu kwa taasisi za umma zinazotumia mwongozo wa 'IPSAS' katika uandaaji wa hesabu kwa mwaka 2020 na leo (Ijumaa, Desemba 3, 2021) kukabidhiwa tuzo na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa  HESLB na Mhasibu Mkuu wa  Serikali CPA(T) Leonard Mkude katika hafla fupi ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa NBAA wa siku tatu iliyofanyika Bunju, jijini Dar es salaam.

Katika kundi hilo, mshindi wa kwanza ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wa pili ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Jumla ya taasisi 71 kutoka sekta binafsi na umma zimeshiriki shindano hilo. Taasisi hizo ziligawanywa katika makundi 13 ya kisekta.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA Prof. Sylvia Temu amesema upatikanaji wa washindi wa tuzo umefanyika kwa kuzingatia vigezo wazi na vya kitaaluma.

Kwa upande wake, CPA (T) Mkude, ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba amezipongeza taasisi zilizojitokeza kushiriki shindano kwa sababu linalenga kuongeza ufanisi.

"Kwa taasisi zote zilizoshiriki, natoa wito zipokee maoni na matokeo ya ushiriki kwa maoni chanya na kuboresha," amesema.

Akizungumzia tuzo hiyo mara baada ya kupokea, Mhasibu Mkuu wa HESLB CPA(T) Brown Obeligwe Shimwela amesema wameipokea kama chachu ya kuongeza ufanisi zaidi.

"Tuzo hii pia ni matokeo ya uboreshaji mifumo ya fedha, mikopo na taarifa za wateja wetu na ushirikiano wa wafanyakazi wote ...tutaendelea kuboresha ufanisi," amesema CPA(T) Shimwela.

Mashindano hayo yalianzishwa na NBAA miaka 10 iliyopita na HESLB ilianza kushiriki mwaka 2018/2019 ambapo ilishika nafasi ya nne (04) kwa taasisi za Serikali zinazoandaa hesabu kwa mwongozo wa 'IPSAS'.

No comments:

Post a Comment

Pages