HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 03, 2021

PROF. NDALICHAKO AVUTIWA NA BUNIFU TAASISI YA TEKNOLOJIA DAR ES SALAAM

Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako,  akitangaza mkusanyiko kuwa mahafali ya 15 ya Taasisi ya Teknoloji Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,  Prof Joyce Ndalichako , akitunuku shahada mbalimbali wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam.

Wahitimu.

 

Na Mwandishi Wetu


Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,  Prof Joyce Ndalichako amesema Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imepewa jukumu la kimkakati katika kuhakikisha inasimamia vizuri uzalishaji wa wataalamu katika fani ya sayansi na ufundi ambao wanatarajiwa kuendesha viwanda kwa weledi.


Prof.  Ndalichako amesema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika mahafali ya 15 ya Taasisi hiyo ambapo alikua mgeni rasmi, ameitaka pia DIT kuhakikisha inafanya mapitio ya mitaala ili kujiridhisha ujuzi unaotolewa unaendana na mahitaji ya sasa ya jamii na soko la ajira.


"Nitumie fursa hii kuwakumbusha DIT kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inawategemea sana wanasayansi na wahandisi katika kufanikisha lengo la kuwa nchi ya uchumi wa viwanda. Aidha Mheshimiwa Rais anasisitiza utoaji wa elimu inayojenga ujuzi," amesema Prof Ndalichako.


Amesema kuwa amefarijika kuona idadi ya wahitimu imeongezeka hatua hii inayoonesha kuwa Taasisi imeimarika kwa kuendelea kuzalisha rasilimali watu katika fani za mafundi sanifu, wanasayansi na wahandisi.


"Nimetaarifiwa kuwa kuna ongezeko la kozi na udahili wa wanafunzi, uboreshaji wa vifaa vya kufundishia na miundombinu katika miaka ya hivi karibuni, haya ni maendeleo mazuri na napenda niwapongeze Baraza na Menejimenti ya Taasisi kwa juhudi hizi ambazo zitasaidia kuandaa wataalam wenye weledi," amesema.


Prof Ndalichako amempongeza pia Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi hiyo, Mhandishi Dkt Richard Masika kwa kwa uteuzi wake huo kuisimamia DIT ambapo amesema ana matumaini kuwa atasimamia kwa makini, ueledi na uaminifu mkubwa Taasisi hiyo kuhakikisha inapiga hatua kubwa ya maendeleo na kufikia ndoto yake ya kuwa Taasisi kinara katika kutatua changamoto mbalimbali za jamii kwani yeye ni mdau mkubwa wa sekta ya elimu ya Ufundi.


Prof Ndalichako amewakumbusha pia wahitimu kuwa baada ya kuhitimu jamii ina matarajio makubwa kutoka kwao kama mafundi sanifu na wahandisi mliosoma katika Taasisi hii maarufu ya DIT hivyo wakaoneshe umahiri na mfano bora mahali pa kazi.


Kwa upande wake Mhandisi Dkt Masika

ameomba pogramu za Ufundi Sanifu kupewe kipaumbele katika mipango ya maendeleo hasa kutoa ufadhili kwa kundi maalum la wanafunzi wa stashahada ya uhandisi ili kuvutia wanafunzi kujiunga kwa wingi sambamba na kuvutia vyuo kuongeza idadi ya wanafunzi hao.


Amebainisha kuwa DIT imepanga kuongeza idadi ya wanafunzi wa ufundi sanifu uhandisi kwa zaidi ya asilimia 50% ya waliodahiliwa hivi sasa iwapo itapata nafasi ya kupanuka kwa haraka.


Amesema takwimu zilizopo zinaonesha kwamba Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa yanapendekeza kuwa uwepo uwiano kwa kila mhandisi mmoja (1) mafundi sanifu (technicians) watano (5) na mafundi stadi (artisans) 25 ili kuleta tija na ufanisi katika shughuli za uzalishaji hasa viwandani uwiano ambao hapa nchini haupo.


"Hakuna dalili za kuukaribia uwiano huu, tukiangalia takwimu za wahitimu wa uhandisi zinalingana na zile za mafundi sanifu au wakati mwingine wahandisi wahitimu ni wengi kuliko wahitimu wa ufundi sanifu, tatizo ni kubwa kwani takwimu za wahitimu hawa wa DIT walioko mbele yako ambao kati yao takribani asilimia 56% tu ndio mafundi sanifu," amesema Mhandisi Dkt Masika.


Katika hatua nyingine amemshukuru Rais Samia kwa kumteua kuwa mwenyekiti wa Baraza la DIT April 16, 2021 na kuahidi kutekeleza wajibu wake kwa bidii, weledi na uadilifu.


"Mimi na Wajumbe wa Baraza la Taasisi tumepewa jukumu kubwa la kusimamia Taasisi hii ya kipekee nchini mwetu, ninaamini kwamba tutashirikiana kuisimamia kwa weledi na kimkakati ili kutekeleza azma ya Rais wetu ya kuhakikisha kwamba Taasisi hii inatoa wataalam ambao watakuza uchumi wa viwanda na kutatua changamoto mbalimbali katika jamii," amesema.


Naye Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam,  Prof Preksedis Ndomba amesema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1004 (ME - 754 KE - 250) wametunukiwa tuzo mbalimbali huku wahitimu wa kike wamepanda kutoka asilimia 21 hadi 25.


"Tunafarijika kuona kuwa wahitimu wa kike wameongezeka kutoka asilimia 21 mwaka jana na kufikia asilimia 25 mwaka huu," amesema Prof Ndomba.


Wahitimu ni Stashahada 568 (ME - 412, KE - 156) Shahada 407 (ME - 317, KE - 90) Shahada ya Kwanza 29 (ME - 25, KE – 4) Idadi ya wahitimu wa kike ni sawa na asilimia 25.


Aidha, amesema DIT imejipanga kuendesha mafunzo yake kiubunifu zaidi kwa kuhusisha mafunzo ya kitaalamu (Training Centre), teknolojia atamizi (technology incubator) na mafunzo kwa vitendo viwandani (teaching factory).

No comments:

Post a Comment

Pages