Hati fungani hii ya NMB Jasiri ni kwa ajili ya wawekezaji wote, wadogo na wakubwa
· Kiwango cha chini cha ununuaji wa hati fungani hii ni TZS 500,000
· Hati Fungani ya NMB Jasiri inaweza kununuliwa kutoka kwenye tawi lolote la Benki ya NMB au kwa madalali wa hisa waliosajiliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa riba ya asilimia 8.5 kwa mwaka.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Hati Fungani Maalum ‘NMB Jasiri Bond’ uliofanyika leo Februari 7, 2022 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Mkuu Wateja Binafsi NMB, Filbert Mponzi na Afisa Mkuu Hazina, Azizi Chacha. (Picha na Habari Mseto Blog).
Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akizindua Hati Fungani Maalum ‘NMB Jasiri Bond’ uliofanyika leo Februari 7, 2022 jijini Dar es Salaam, huku maofisa wa ngazi za juu wa benki hiyo wakishuhudia. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi, Aikansia Muro, Afisa Mkuu wateja Binafsi, Filbert Mponzi, Afisa Mkuu Hazina, Azizi Chacha na Afisa Mkuu Huduma Shirikishi, Nenyuata Mejooli.
Dar es Salaam, Februari 7, 2022. Benki ya NMB imetangaza kuanza kuuzwa rasmi kwa hati fungani ya miaka mitatu inayomlenga mwekezaji yeyote aliye tayari kuwekeza katika taasisi hiyo kwa ajili ya kupata riba nzuri.
Kiwango cha chini cha uwekezaji kwenye hati fungani hii ni TZS 500,000 na itaweza kununuliwa kutoka kwenye tawi lolote la Benki ya NMB au kwa madalali wa hisa waliosajiliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Hati fungani hii ya NMB Jasiri inategemea kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 25 kupitia mauzo ya dhamana hii,lakini ikiwa na kipengele cha kuongeza TZS bilioni 15 zaidi.
Mapato ya Hati fungani hii ya NMB Jasiri yatatumika kusaidia utoaji wa mikopo kwa biashara na makampuni yanayomilikiwa au kusimamiwa na wanawake pamoja na biashara ambazo bidhaa na ama huduma zake zinamnufaisha mwanamke.
Hii ni hati fungani ya kipekee na ya kwanza kutolewa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi na inaendelea kuonyesha tu jinsi Benki ya NMB inavyoendelea kuunga mkono juhudi za kufikia Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hasa lengo endelevu namba 5 (SDG 5) linalohusu Usawa wa Kijinsia na lile la namba 10 (SDG 10) lililojikita katika kupunguza tofauti za kijinsia.
Wawekezaji kwenye hati fungani hii watapata riba ya asilimia 8.5 kwa mwaka itakayolipwa kila robo mwaka wakati wa kipindi chote cha miaka mitatu mpaka mwezi Machi mwaka 2025. Riba itakayolipwa itakatwa kodi ya zuio.
Uuzwaji wa Hati fungani hii ya NMB Jasiri umepata kibali kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) walioruhusu awamu ya nne ya Programu ya NMB ya Utoaji wa Hati Fungani ya Muda wa Kati yenye thamani ya TZS bilioni 200 (NMB Plc TZS 200bn/- Medium Term Note (MTN) Programme). Awamu tatu zilizotangulia za programu hii, zimepelekea kupatikana kwa TZS bilioni 148.2.
Kipindi cha ofa kikimalizika (21 Machi 2022), Hati fungani hii itaorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Hii maana yake ni kuwa mnunuzi wa hati fungani hii atakuwa na uwezo wa kuiuza hati fungani hii kwa mnunuzi mwingine kupitia kwa mawakala wa Soko la Hisa na kupata fedha yake aliyowekeza kabla ya muda wa Hati fungani kuiva.
Kwenye maandalizi ya kuileta sokoni Hati fungani hii, Benki ya NMB ilishirikiana na kampuni za FSD Africa na Sustainalytics; kampuni hizi zilitoa ushauri wa kitaalam ambao unaifanya Hati fungani hii kukidhi vigezo na viwango vya kimataifa kwa mujibu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji (ICMA).
Katika utoaji wa hati fungani hii, NMB pia imeshirikiana na kampuni ya Orbit Securities ambayo ndiye wakala mdhamini wa hati fungani hii.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza kufunguliwa kwa hati fungani hii, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB - Ruth Zaipuna amesema: “Kimsingi NMB inapata fedha za kufanyia shughuli zake za kibiashara kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo amana ndogo ndogo na kubwa, pamoja na kupitia vyanzo kama Hati Fungani hii ya NMB Jasiri.
“Mtakumbuka kuwa tuna Programu ya Utoaji wa Hati Fungani ya Muda wa Kati (MTN) ya TZS bilioni 200 na mpaka sasa tumeweza kutoa mafungu matatu (3) yenye thamani ya jumla ya TZS bilioni 148.2.
“Kupitia Hati fungani hii mpya ya NMB Jasiri, NMB inatarajia kukusanya TZS bilioni 25 ambazo zitaenda moja kwa moja kusaidia utoaji mikopo kwa kampuni au biashara zinazomilikiwa au kuongozwa na wanawake. Hati fungani hii ina nafasi ya ongezeko la TZS bilioni 15.
“Wanawake wana mchango mkubwa na muhimu katika ukuaji endelevu wa uchumi na ustawi wa pamoja huku wakiwa na majukumu ya msingi katika nyanja zote za maisha ya jamii na ya kibinafsi.
“Kupitia Hati fungani hii ya NMB Jasiri, tunaonyesha kwa vitendo jinsi ya kutatua changamoto za wanawake wajasiriamali wa Tanzania wanazokabiliana nazo huku tukianzisha rasilimali mpya kwa wawekezaji ambao wanataka kusaidia kuwepo suluhisho endelevu kwenye uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, wanawake ni zaidi ya nusu ya watu wote duniani. Biashara nyingi ndogo na za kati zinamilikiwa na wanawake, lakini wengi hukabiliwa na vikwazo vingi kupata mikopo kutoka benki, hii ikimaanisha biashara zao haziwezi kukua kama inavyostahili.”
“Kwetu sisi hii ni fursa ya kukabiliana na changamoto hii ambayo pia itasaidia kuchochea maendeleo ya soko la mitaji la ndani na kupanua wigo wa vyanzo vyetu vya kifedha huku ikiwawezesha wanawake kiuchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa ujumla. Hii ni fursa inayotuwezesha kupanua zaidi Jukwaa letu la Wanawake la Jasiri lililozinduliwa mwaka 2020.”
“Aina hii ya hati fungani pia hutoa fursa kwa wawekezaji wadogo kuwekeza katika dhamana za (viwango vidogo) kiasi kidogo, kupanua wigo wa uwekezaji na kushiriki katika soko la hati fungani hivyo kuongeza ushirikishwaji kifedha na ufikiaji huduma unaostahili kwa kutumia mtandao wa benki yetu unaopatikana kirahisi.”
“Uuzaji wa Hati Fungani ya NMB Jasiri utaanza leo Februari 7, 2022, hadi Machi 21, 2022. Maombi yote ya kuinunua Hati fungani hii yatapita kwenye matawi yote 226 ya NMB au kwa madalali waliosajiliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).” Alisema Bi Zaipuna
Mkurugenzi wa Masoko ya Mitaji kutoka FSD Afrika alisema kuwa “FSD Afrika ina furaha kubwa kufanya kazi na Benki ya NMB kuweza kuleta Hati fungani hii ya NMB Jasiri ambayo ni ya kwanza kuwahi kutolewa katika ukanda wa Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara. Hati fungani hii itasaidia sana kuwawezesha wanawake kiuchumi na itatengeneza fursa mpya kwa wawekezaji wadogo na hata taasisi na makampuni nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.”
No comments:
Post a Comment