Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akitoa tamko katika Maadhimisho ya siku ya Saratani Duniani kwa mwaka 2022 yenye kauli mbiu isemayo "Huduma za Saratani Sawa kwa Wote".
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
TATIZO la ungonjwa wa saratani linakadiriwa kuongezeka na kwamba idadi ya wagonjwa wapya kufikia milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Pia takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (International Atomic Research on Cancer-IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kwamba kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani kila mwaka ambao ni sawa na takribani asilimia 50.
Hayo yameelezwa leo Februari 04 jijini Dodoma na Waziri wa afya Ummy Mwalimu wakati akitoa tamko katika Maadhimisho ya siku ya Saratani Duniani kwa mwaka 2022 yenye kauli mbiu isemayo "Huduma za Saratani Sawa kwa Wote".
Amesema takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zinaonyesha kuwa tatizo la saratani nchini Tanzania limekuwa likiongezeka siku hadi siku ambapo inakadiriwa kuwa katika kila watu100,000, watu 76 hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani.
Waziri Ummy ameeleza kwamba Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo.
"Takwimu kutoka kwenye kanzi data (Population based Cancer Registry) zilizo anzishwa kwa Kanda,zinaonesha kwamba wagonjwa wapya 14,136 walifikiwa na huduma ambayo ni sawa na asilimia 33 ya makadirio ya wagonjwa wapya wote kwa mwaka 2021 ikiwa niongezeko la asilimia tano ukilinganisha na takwimu za Mwaka 2020 ambapo jumla ya wagonjwa wapya 12,096 sawa na asilimia 28 walionwa," amesema.
Amefafanua kuwa taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume Prostate cancer asilimia 21 Saratani ya Koo (Esophageal Cancer) asilimia 11.8, Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo asilimia 9 na Saratani ya mdomo na kinywa asilimia 7.3.
Waziri huyo amelelewa kuwa kwa upande wa wanawake saratani zinazowaathiri zaidi ni pamoja na Saratani ya Mlango ya Kizazi (Cervical Cancer), asilimia 43, Saratani ya Matiti (Breast Cancer) asilimia14.2 na Saratani ya koo asilimia3.8.
Waziri Ummy amesema kuwa ongezeko la wagonjwa wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia afya bora kama kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi.
Amesema kuwa serikali imeongeza juhudi za kuhakikisha kuwa uelewa katika jamii kuhusiana na tatizo hilo unaongezeka kwa kuandaa mtaala wa mafunzo mashuleni unaozungumzia magonjwa yasiyoambukiza na namna ya kudhibiti.
Waziri Ummy amesema serikali pia imeanzisha Program ya taifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa Yasiyoambukiza ikiwa ni jitihada za kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani.
"Mpango wa Taifa kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wameandaa kitini cha Mtindo wa Maisha kinachoelezea magonjwa haya na namna ya kujikinga na kudhibiti kwa wale waliokwisha athirika," amesema waziri Ummy.
Amesema sambamba na hilo Tanzania imetunga Sheria mbalimbali,miongozo na mikakati ya udhibiti wa vihatarishi ili kuweza kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
Waziri huyo ameongeza kuwa karibu theluthi moja ya Saratani zinaweza kutibika endapo mgonjwa atabainika mapema, hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya kampeni maalum na kuhimiza wananchi kufanya uchunguzi wa Afya zao ili kubaini ugonjwa katika hatua za awali.
Ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita imehakikisha huduma za kinga na matibabu ya saratani zinapatikana nchini na kwamba vituo vya uchunguzi na matibabu ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi zaidi ya 800 vimefunguliwa nchi nzima kuanzia kwenye ngazi ya Zahanati hadi kwenye ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda.
"Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 51.5 ikilinganishwa na vituo 350 vilivyokuwepo kwa mwaka 2015 na Mafanikio haya yamepelekea serikali kuweza kutoa huduma za uchunguzi za saratani ya mlango wa kizazi kwa Jumla ya wanawake 513,375 sawa na ongezeko mara nne idadi ya wanawake127, 188 waliopatiwa huduma hizo mwaka 2015.
"Serikali imeimarisha huduma za kibingwa katika hospitali 6 za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya Uchunguzi na Tiba kwa kuongeza wataalam, miundo mbinu na Vifaa Tiba," ameongeza.
Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa Saratani tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya," amesema.
Amefafanua kuwa kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya Saratani lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa wa Saratani na kwa wale ambao hawajapata ugonjwa huu waendelee kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za Mtindo bora wa maisha.
"Naomba kuweka msisitizo kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza hususan saratani kwa kufanya yafuatayo
kuzingatia ulaji unaofaa kwa kula mlo kamili, ulaji wa matunda na mboga mboga za kutosha, kuepuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, kuepuka kula vyakula vyenye chumvi nyingi, na kuepuka ulaji wa vyakula na vinjywaji vyenye sukari nyingi," amesema.
No comments:
Post a Comment