HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 07, 2022

TEA, BRAC watoa kompyuta 120 shule za Temeke



Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Elimu Tanzania kwa kushirikiana na asasi ya BRAC-Maendeleo wametoa kompyuta 120 zenye thamani ya Sh milioni 132 kwa shule tatu za Wilaya ya Temeke kwenye mradi wa “Skills for Their Future”.

Kompyuta hizo zilikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo kwenye hafla iliyofanyika jana katika shule ya sekondari Karibuni iliyoko Temeke Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Shule za sekondari zitakazonufaika na kompyuta hizo ni Miburani, Wailes na Karibuni.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Jokate alisema  makubaliano baina ya BRAC - Maendeleo Tanzania na TEA ni mfano wa namna taasisi za umma na zile zisizo za kiserikali au binafsi zinavyoweza kufanya kazi kwa pamoja katika kuboresha maisha ya wananchi.

 
Jokate alisema TEA inafadhili ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, mabweni, mabwalo namajiko yake, maabara na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika ngazi zote za elimu Tanzania Bara na ngazi ya Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar.

 
“Nichukue nafasi hii kuwasilisha shukrani za dhati kwa Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania chini ya Mkurugenzi Mkuu, Bahati Geuzye, Wilaya ya Temeke ni miongoni mwa Wilaya zinazonufaika na Miradi inayofadhiliwa na TEA,” alisema

Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye alisema mamlaka hiyo imeshakarabati shule kongwe 17 za sekondari kati ya 89 zilizopo katika mpango huo wa ukarabatina hivi karibuni ilishiriki kukarabati shule nne za msingi mkoani Dodoma.

 
Alisema kutolewa kwa kompyuta hizo ni uzinduzi wa mradi wa ‘Skills for Their Future’  unaolenga kutoa mafunzo ya kidijitali kwa vijana wa shule za sekondari ili kuwawezesha kupata ujuzi na stadi zitakazosaidia kuboresha maisha yao.

 
“Kompyuta hizi zinatolewa baada ya kusainiwa kwa makubaliano maalum ya ushirikiano baina ya TEA na BRAC-Maendeleo ikiwa ni mkakati wa kuunga mkono serikali wanafunzi kujifunza kupitia TEHAMA katika ngazi zote za elimu nchini,” alisema.


 Alisema kompyuta hizo zitanufaisha wanafunzi 1,800 na walimu 45 na kwamba ni matumaini kwamba wanafunzi wa shule hizo tatu watatumia vizuri fursa ya miundombinu hiyo ya kompyuta kupata maarifa na taaluma zitakazowawezesha kufanya vizuri kwenye masomo yao.

 
Alisema walimu nao watatumia fursa hiyo kuboresha ufundishaji wa masomo na hivyo kusaidia shule zao kufanya vizuri kitaaluma na kwamba TEA inafarijika kuona wadau wa maendeleo kama BRAC wanatoa mchango wao kupitia mamlaka ya elimu.

 
Mkurugenzi Mkuu wa BRAC-Maendeleo, asasi hiyo imeichagua wilaya ya Temeke katika kutekeleza miradi mbalimbali na wameshirikiana na wilaya kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu.

 
 “Tunawashukuru viongozi wa Wilaya hii kila tunapokuja kuanzisha mradi mpya mnatupokea vizuri na mnatupa ushirikiano mkubwa nawapongeza sana na tunafanya hivi kwenye maeneo mengi nchini,” alisema
 

Alisema mbali na mradi huo wanatekeleza miradi mingine ya usalama na chakula uwezeshaji kwa vijana na wanawake na katika mradi huo wamefanya mambo mengi wilaya ya Temeke.

No comments:

Post a Comment

Pages