HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 07, 2022

WFP yawawezesha wakulima wa mtama kupata bil.13.5/-

 

Na Mwandishi Wetu, Bahi

WAKULIMA wa mtama wa Wilaya sita za Mkoa wa Dodoma, wamenufaika na mradi wa kilimo himilivu cha zao hilo (CSA) unaosimamiwa na Shirika la Farm Africa na kuwezeshwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

Kwa mujibu wa WFP, kupitia mradi huo wakulima hao katika msimu wa mwaka 2020/2022 wamevuna tani 28,000 za mtana uliowaingizia Sh.bilioni 13.5.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma, Mkuu wa Ofisi Ndogo ya WFP iliyopo jijini hapa, Neema Sitta amesema mradi huo umeleta tija kubwa kwa wakulima ambao kwa sasa mbali ya kuvuna mtama mwingi pia wamekuwa na soko la uhakika na kuondoa changamoto
ya soko kwa zao hilo.

"Mradi wa CSA unatekelezwa katika vijiji zaidi ya 200 vilivyopo kwenye Wilaya sita za Mpwapwa, Chamwino, Bahi, Kongwa, Chemba na Kondoa ambapo kwa msimu wa mwaka 2020 hadi 2021 wamefanikiwa kuuza zaidi ya tani 28,000 za mtama, zenye thamani ya Sh. bilioni 13.5,”alisema Neema.

Aidha alisema kuwa mradi huo licha ya kusimamiwa na WFP lakini unadhaminiwa na Shirika la maendeleo la Ireland (IrishAid).  

"Mradi huu ni wa gharama ya shilingi bilioni 1.7 na umegusa wakulima zaidi ya 22,000 ambao wapo kwenye mradi kutoka katika wilaya hizo sita lakini pia umenufaisha ya watu 100,000 ndani ya mkoa wa Dodoma,” alisema Neema.

Aidha Sitta amesema matarajio yao ni kuona wakulima wa mtama wanaongeza uzalishaji katika msimu huu mpya wa kilimo na WFP wako tayari katika kuhakikisha wanashirikiana kikamilifu na wakulima hao wa mtama.

“Tuliweka mkazo kwenye zao hili la mtama kwa sababu zao hilo kukubali kwenye ardhi na mazingira ya Dodoma, pamoja na uhakika wa soko, unajua mazingira ya Dodoma ni yenye ukame na mvua kidogo" aliongeza kusema.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa kilimo himilivu cha Mtama kutoka Shirika la FarmAfrica Tanzania  wanaoendesha mradi huo, Grace Changanyika amefafanua kupitia mradi huo wakulima wa mtama wamepiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Alisema maendeleo ya mradi huo yanatokana na kuwepo kwa soko la mtama la uhakika ambapo wanunuzi wakubwa ni pamoja na Kamuni ya bia Tanzania (TBL) ambao wanaendesha kilimo cha kimkataba.

“TBL ni miongoni mwa wanunuaji wakubwa wa mtaa ambapo Kampuni hiyo inaingia mkataba na wakulima kwa ajili ya kununua mtama wote unaozalishwa kupitia mradi huu, hii imeongeza tija kwa wakulima ambapo kwa sasa hawana wasiwasii wa soko,” alisema Grace.

Alisema pia wapo wanunuzi wengine wa ndani ya nchi lakini pia zao hilo lina soko kubwa kwenye nchi ya Sudan Kusini ambapo mfanyabiashara na msafirishaji Ali Juma amekuwa akinunua na akipeleka mtama nchini humo.

“Kuwepo kwa mnunuzi kama TBL na wengine wamefanya bei ya mtama kwa wakulima kuwa ya kuridhisha kwa sababu kwa sasa bei sokoni ni sh, 550 kwa kilo moja ambapo ni tofauti na bei ya awali kabla ya mradi ambapo mtama ulikuwa unauzwa kati ya 250-300 kwa kilo,” aliongeza kusema Afisa Mradi huo.

Wakati huo huo, baadhi ya wakulima wa zao hilo wameishukuru WFP na FarmAfrica kwa kuwapelekea mradi huo ambao umewawezesha kubadilisha maisha yao.

Mmoja ya wakulima hao Patrick Mbeho ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Mkola Wilaya ya Bahi amesema mradi huo umemletea mapinduzi makubwa kwenye maisha yake kwa kupata mafaniko makubwa.

“Kwangu haya ni mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo kwani nilikuwa napata Sh. milioni mbili kwa shamba la hekari 20 ila kwa sasa baada ya kuingia mradi huu na kupata elimu napata hadi Sh. Milioni sita mpaka saba , umenifanya nimejenga nyumba ya biashara,nimenunua mashine ya kupembulia mtama na mengine mengi,” alisema Mbeho

Kauri hiyo iliungwa mkono na mkulima mwingine wilayani humo Shabani Lukupe ambaye amesema awali walikuwa wakilima mtaama kwa ajili ya chakula lakini ujio wa madi huo na elimu waliyoipata wamegeuza kilimo hiko kuwa cha kibiashaara na kufanikiwa kupata pesa zinazokidhi mahitaji ya familia ikiwa pamoja na kusomesha watoto, kujenga nyumba za kisasa pamoja na kuwa na uhakika wa chakula.

No comments:

Post a Comment

Pages