Maroli yanayosafirisha bidhaa kwenda Kenya yakwama.
Na Benny Mwaipaja
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa Serikali itawasiliana na Mamlaka za Kenya ili kutatua changamoto ya malori ya mizigo yanayovuka kupeleka bidhaa nchini humo kutumia muda mrefu kupata vibali vya kuvuka mpaka wa Horohoro-kuingia Kenya.
Dkt. Nchemba alisema hayo baada ya kuzungumza na madereva wa malori yanayobeba shehena ya mizigo kwenda Kenya katika Mpaka wa Horohoro, akiwa njiani kwenda Mombasa-Kenya, kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Madereva hao walieleza kuwa wanapata usumbufu mkubwa kwa sababu wanatumia muda mrefu unaokadiriwa kufikia hadi siku 14 hadi 21 kuvuka mpaka wa Horohoro kwenda nchini Kenya, wakati upande wa madereva wa Kenya wanaoingia Tanzania wanatumia siku zisizozidi 3 kuvuka mpaka huo.
Walimweleza Dkt. Nchemba kwamba, kuchelewa kuvuka mpaka kunawaletea matatizo makubwa ikiwemo kutumia gharama kubwa zisizolingana na posho za safari wanazopewa na waajiri wao, lakini pia kuna baadhi ya bidhaa zinaharibika kabla ya kuvuka mpaka.
Dkt. Nchemba alisema amebaini kuwa ucheleshwaji wa huduma ya forodha kwa Kenya unatokana na nchi hiyo kutoanza kutumia Mfumo wa Pamoja wa Huduma ya Forodha (Single Custom Territory) kama walivyokubaliana.
Alisema kuwa magari ya Kenya hayapati changamoto hiyo ya foleni kwa kuwa Tayari Tanzania wanatumia mfumo huo ambapo mizigo yote ya Kenya hupata vibali ikiwa huko huko nchini Kenya, kabla ya kufika katika mpaka huo wa Horohoro na malori kupita bila tatizo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa atawasiliana na Waziri mwenzake wa Fedha wa Kenya ili kuanza kutekeleza makubaliano ya kuweka Mfumo huo wa Pamoja na Forodha kwa kuwapeleka watumishi wa nchi hiyo upande wa Tanzania ili kuharakisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka Tanzania hivyo kuwaondolea adha wafanyabiashara na madereva wanaotumia mpaka huo kufanya biashara zao.
No comments:
Post a Comment