HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 22, 2022

Mjumita, TFCG wataka changamoto USMJ zitatuliwe


 

 Mkurugenzi Mtendaji wa Mjumita, Rahima Njaidi akifuatilia mada kuhusu umuhimu wa usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii, katika mkutano wa wadau wa sekta hiyo uliofanyika mjini Morogoro, kulia kwake ni maofisa kutoka Serika.

 


Mwenyekiti wa Mjumita, Rehema Ngelekele akifuatilia mada kuhusu fauda za usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii katika mkutano wa wadau wa sekta hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Morogoro.

 

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

 

MTANDAO wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), wamewaomba viongozi wa Serikali za vijiji na taifa kutatua changamoto za Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ), ili kuifanya misitu kuwa salama.

Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mjumita, Rahima Njaidi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusikiliza maelezo ya wadau wa usimamizi wa misitu  jamii, walioshiriki mkutano ulioitishwa na taasisi hizo mwishoni mwa wiki mjini Morogoro.

Njaidi alisema TFCG na MJUMITA wamekuwa wakitekeleza mradi wa USMJ katika vijiji 38 vya wilaya saba na mikoa mitatu kwa takribani miaka 10,  hivyo wanaomba wananchi na viongozi kuwa kitu kimoja ili mradi huo uweze kuendelea.

“Tumetekeleza mradi katika vijiji 20 wilani Kilosa, 10 Mvomero na vitano Morogoro Vijijini mkoani Morogoro, Mkoa wa Iringa tuna kijiji kimoja Wilaya ya Kilolo, Lindi tuna kijiji kimoja kimoja katika Wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Liwale,”alisema.

Alisema mradi huo umesaidia wananchi kupata maendeleo, hivyo vijiji na halmashauri wanapaswa kuwa wamoja kuendeleza pale ufadhili utakapofikia kikomo.

“Tumewasikiliza watekelezaji wanavyoelezea changamoto ambayo wanakutana nayo, hasa kwa kuingiliwa na baadhi ya viongozi wasio jua faida za uhifadhi na wanataka kunufaika na miradi hiyo wao binafsi,” alisema.

Alisema wao wataendelea kutoa elimu kwa makundi yote ili kuhakikisha mradi huu unakuwa endelevu na kuchochea maendele.

Njaidi alisema iwapo pande zote zinazokinzana zitakaa pamoja na kujadili kwa kuheshimiana migogoro au changamoto zingepata ufumbuzi.

Mwenyekiti wa MJUMITA, Rehema Ngelekele alisema wao kama mtandao wanashukuru kuona malengo waliojiwekea yamekuwa yakitimia kwa asilimia kubwa.

“Lengo la miradi hii ni kuhifadhi misitu ili isiharibike, kusaidia Serikali kutekeleza miradi ya elimu, afya, kukuza uchumi na maendeleo na kusema ukweli mafanikio ni makubwa,” alisema.

Ngelekele alisema wanaishukuru Serikali kuendelea kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imekuwa ikiinua wananchi kiuchumi na maendeleo.

Naye Mjumbe wa MJUMITA Kanda ya Mashariki Juliana Mwenda, alisema mtandao huo kwa kushirikiana na TFCG wameweza kugusa maisha ya wananchi kupitia miradi ya USMJ.

“Zipo changamoto za miradi kutokuwa na mwelekeo mzuri wa kuwa endelevu, hivyo tunaomba Serikali itenge bajeti ambayo itawezesha vijiji vinaendeleza miradi ya uhifadhi kwani ina faida kwa wananchi,” alisema.

Aidha, Mwenda alitoa rai kwa Serikali kuzingatia sheria na kanuni pale ambapo zinataka kuchukua hatua kwa  kamati za maliasili za vijiji.

Kwa upande wake Ofisa Misitu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sanford Kway alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kama Mjumita na TFCG ambao wamekuwa wakitoa elimu ya uhifadhi misitu kwa njia endelevu.

Kway alizitaka mamlaka za Serikali za mitaa kuendeleza miradi hiyo kwa kuanzisha mradi katika vijiji vingine ambavyo vina misitu yenye asili ya uendelevu baada ya kuvunwa  na sio kuchochea migogoro.

“Miradi hii kwa vujumla wake imekuwa na faida kubwa kwa maeneo ambayo inatekelezwa, sisi Tamisemi hatuko tayari kuona mafanikio haya yanaharibiwa,” alisema.

Awali wananchi na viongozi wa vijiji ambavyo vipo kwenye mradi wa USMJ walieleza changamoto wanazokutana nazo ni pamoja na kamati za maliasili kuingiliwa, rushwa na tamaa.


No comments:

Post a Comment

Pages