HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 11, 2022

PURA kushiriki Maonesho ya NEEC Morogoro

 Watanzania kunufaika na elimu kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia

Mjiolojia Fortunatus Kidayi (kulia) akizungumza na mshiriki wa Maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi aliyetembelea banda la PURA. Maonesho hayo yanafanyika viwanja vya Jamhuri mkoani Morogoro.

 

 Na Janeth Mesomapya

 

Watanzania wanatarajiwa kunufaika na elimu kuhusu sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia itakayotolewa na wataalamu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwenye Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi mkoani Morogoro.

 

Wataalamu hao wamejipanga kukuza uelewa wa sekta hiyo ili kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye sekta husika.

 

Maonesho hayo yamefunguliwa Mei 9, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Martin Shigela katika viwanja vya Jamhuri mkoani humo na yataendelea hadi Mei 14, 2022 ambapo yanatarajiwa kuhitimishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Baadhi ya masuala yatakayozungumziwa kwenye banda la PURA ni pamoja na mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia, mnyororo wa thamani wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zinazoendelea nchini.

 

Maeneo mengine ni ushiriki wa wazawa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli na fursa zinazopatikana kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Mhe. Shigela amesema maonesho hayo ni fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kazi na washiriki wengine kuhusu fursa mbalimbali na changamoto zinazowakabili na jinsi ya kukabiliana nazo.

 

“Maonesho haya ni ya muhimu kwani yanatoa elimu kwa wananchi ambayo inawawezesha kushiriki kwa wingi na kwa ubora kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo,” alisema.

 

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng'i Issa amesema maonesho hayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “uchumi imara kwa maendeleo endelevu”.

 

Aliongeza kuwa lengo la maonesho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu uwepo wa mifuko na programu za uwezeshaji, jinsi ya kujiwekea akiba na jinsia ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.

 

“Maonesho haya pia yanalenga kutengeneza mtandao wa wafanyabiashara watakaoshiriki na kukuza masoko ya wajasiriali ili kujiletea maendeleo,” alibainisha.

 

No comments:

Post a Comment

Pages