HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 11, 2022

TWAWEZA YAPONGEZWA KWA UBUNIFU KATIKA SEKTA YA ELIMU

 

Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akizungumza katika Sherehe ya kuwatunuku walimu mahiri bakshishi ya KIUFUNZA awamu ya tatu (2019-2021) unaoratibiwa na Twaweza.


Na Asha Mwakyonde, Dodoma

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amelipongeza Shirika la Utafiti Tanzania (TWAWEZA) kwa kubuni mfumo  wa KiuFunza ambao utachochea walimu kuongeza ubunifu katika kazi zao wawapo darasani kuongeza uboreshaji wa elimu zaidi hapa nchini.

KiuFunza ni malipo ya walimu kulingana na utaendaji  ni mfumo wa motisha unaounganisha malipo ya bakshishi kwa walimu na viwango vya ujuzi wanavyofikia wanafunzi wao katika kusoma,kuandika  na kuhesabu (KKK).

Akizungumza jijini Dodoma Mei 7,2022, wakati akifungua sherehe za kuwatunuku walimu Mahiri bakshishi ya KiuFunza,2022 ambayo imeandaliwa na Twaweza kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Mkenda  amesema kuwa Tanzania inahitaji kuwa na Elimu bora na sio bora elimu kwa kuongeza ubunifu katika maeneo ya kujifunzia na kuweka hamasa kwa walimu hao ili kuwaongezea morali katika kazi zao.


Prof. Mkenda amesema kuwa katika kuhakikisha maboresho ya elimu yanafanyika wizara inaendelea kupitia baadhi ya Sera, Sheria na Mitaala iliyopo  na kupunguza au kuongeza mambo muhimu ili kufanya elimu hiyo iendelee kuwa bora zaidi.

Waziri huyo ameongeza kuwa wizara hiyo itahakikisha kuna kuwepo na mazingira salama ya kujifunzia na ya kufundishia (Miundombinu na Vitendea kazi) ambapo kwa hapa Serikali imeshapiga hatua kubwa.

"Ukiwa na walimu wenye ubora ni lazima elimu itakuwa bora  nawapongeza Twaweza kwa kuja na mfumo huu wa KiuFunza ambapo utachochea kila mwalimu kuongeza ubunifu katika kazi yake awapo darasani na  hii itasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wetu," amesama.

Amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa ubora wa elimu unakuwepo nchini wameandaa mkutano wa nchi za umoja wa Afrika Mashariki  mwishoni mwa mwezi Juni  na mawaziri wa elimu pamoja  na wataalamu wa sekta hiyo kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Ureno,Pakistan, South Africa, Kenya,Sierra Leone  wenye lengo la kuzungumzia ubora wa elimu na kupata uzoefu wa mataifa mengine katika sekta ya elimu.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, Mwezi wa Tisa kutakuwepo na Mkutano wa wakuu wa nchi  wa kimataifa  wa Elimu kujadili Mageuzi ya Elimu Duniani.

Naye  Mkurugenzi wa Twaweza, Aidani Eyakuze, amesema kuwa wameona program KiuFunza  ina  manufaa hasa pale ambapo stadi za maisha ndio msingi wa maisha na kwamba motisha hiyo inampa nguzu zaidi  na za ziada mwalimu kufundisha.

"Tumeona mbali miaka 9 ya kufanya majaribio ukimpa mwalimu ahadi mwisho wa mwaka watoto wake wanaendelea vizuri katika stadi za msingi atapata bakshishi," amesem Mkurugenzi wa Twaweza.

Ameongeza kuwa waneona walimu wanajituma kufundisha hata kama ni katika mazingira magumu ndio maana wamekuja na program hiyo.

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo wa KiuFunza kutoka  Mkoani Songwe Michael Kamukulu amesema kuwa utekelezaji wa  mpango huo ni kuishawishi Tanzania kuweka fungu la motisha kwa walimu.

No comments:

Post a Comment

Pages