HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 07, 2022

BUNGE LA WANANCHI LAITAKA SERIKALI KUBADILISHA KIKOKOTOO CHA MAFAO YA WASTAAFU

 

Spika wa Bunge la Wananchi, Celestine Simba, akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupinga kanuni mpya za kikokotoo cha mafao ya wastaafu.  

 

BUNGE la Wananchi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limeitaka serikali kubadilisha kikokotoo cha mafao ya mkupuo na kiwe asilimia 75.

Limesema kuwa kikotoo kilichowekwa sasa kinakwenda kuwaumiza wastaafu.

Mei 26, mwaka huu serikali ilitangaza kiwango kipya cha kikotoo cha mafao ya mkupuo ambapo sasa ni asilimia 33 kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kitaanza kutumika Julai Mosi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Profesa Jamal Katundu, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya makubaliano kati ya Serikali, Chama cha Waajiri Nchini (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) bada ya kusitishwa kwa kanuni zilizotengenezwa Desemba 28 mwaka 2018.

"Makadirio ya miaka 12.5 ya kuishi baada ya kustaafu kama ilivyokuwa kwa mfuko wa NSSF na iliyokuwa PSPF na LAPF," alisema.

Alibainisha kuwa, mshahara wa kukotolea mafao ya pensheni utakuwa wastani wa mishahara bora ya miaka mitatu ndani ya miaka 10 kabla ya kustaafu, huku umri wa kustaafu kwa lazima utaendelea kuwa miaka 60.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Spika wa Bunge hilo la Wananchi, Celestine Simba alisema kuwa kitendo cha serikali kupunguza kikokotoo hicho, kunafanya maisha ya wastaafu kuwa magumu zaidi.

“Kumekuwa na kanuni za kukokotoa mafao ya wastaafu ambazo zimekuwa zikibadilika kulingana na Rais anayekuwepo madarakani. Na hii imefanya suala la mafao kwa wastaafu lionekane kwamba ni hisani ya Rais aliyeko madarakani kwa wastaafu,” alisema.

Alisema kuwa inatakiwa ifahamike fedha hizo zilizoko katika mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii ni michango ya mishahara ya watumishi wa umma inayokatwa kutoka katika mishahara yao kila mwezi, na lengo lake ni kuwasaidia hawa watumishi waweze kuishi vizuri katika ustaafu wao.

“Lakini kilichopo ni kwamba inapofika huyu mtumishi aliyetumikia muda mrefu akastaafu, utata unaanza ambapo fedha zake zinageuka za serikali na kuzipata inakuwa hisani,” alisema na kuongeza kuwa:

“Angalau awamu ya tatu ya Hayati Benjamini Mkapa walau wastaafu walipata nafuu ya kupata kikokotoo cha asilimia 50 kwa mkupuo. Kushusha kwa mafao ya wastaafu kunafanya maisha yao kuwa magumu zaidi, Bunge la Wananchi tumesema hatuwezi kufumbia macho kitendo hiki kwani hakikubaliki kabisa,”.

Alifafanua kuwa, wanapendekeza hivyo kwasababu ni fedha zao, na siziwe mtaji wa mifuko ya Hifadhi za Jamii, badala yake imnufaishe mstaafu.

“Kwa nia njema kabisa tunapendekeza itumike kanuni ambayo ilikuwa nafuu kwa wastaafu ambayo ni awamu ya tatu, kanuni hii itumike katika pensheni na kiinua mgongo….kiwango cha mkupuo ilikuwa asilimia 50, lakini sisi tunapendekeza ipande na kufikia asilimia 75.

“Serikali iwaboreshee kwasababu wanastahili, hebu fikiria kwa miaka sita huyu mfanyakazi hajaongezwa mshahara, amekuja kuongeza mshahara kama hisani ya Rais aliye madarakani. Halafu ndani ya miaka sita hajaongezwa mshahara inaangukia kwenye ustaafu wake, anataka kuchukua mafao yake anapewa asilimia 33 tu ya pesa yake iliyopo,” alisema na kuongeza kuwa:

“Mfanyakazi huyu baada ya kustaafu anaishi miaka mitatu tu anafariki, hatuwatendei haki wastaafu wetu. Hivyo ni lazima tupige kelele kuhusu jambo hili. Tunataka wastaafu wetu waheshimiwe kwasababu hizo fedha ni za kwao, wapewe,”.

Hata hivyo alisema wanajipanga kupeleka mapendekezo yao hayo, sehemu husika ili yaweze kufanyiwa kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages