HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 01, 2022

DIT KUANZISHA KOZI YA UHANDISI TIBA


Kaimu Naibu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam,  Profesa Christopher Mgonja kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), akifungua mkutano wa wadau waliokutana kwa ajili ya kufanya mapitio ya mtaala wa Stashahada ya Nishati Jadidifu (Ordinary Diploma in Renewable Energy -NTA Level 4&6) na kuandaa mtaala mpya wa Shahada ya Kwanza ya Uhandisi Tiba (Bachelor of Engineering in Biomedical Engineering -NTA Level 7&8).

Mkuu wa Idara ya Uhandisi Umeme kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ( DIT), Dkt. Godfrey Moshi  akifafanua jambo katika mkutano wa wadau walioketi kwa ajili ya kufanya mapitio ya mtaala wa Stashahada ya Nishati Jadidifu (Ordinary Diploma in Renewable Energy -NTA Level 4&6) na kuandaa mtaala mpya wa Shahada ya Kwanza ya Uhandisi Tiba (Bachelor of Engineering in Biomedical Engineering -NTA Level 7&8).
 


NA MWANDISHI WETU


TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) inafanya mapitio ya mtaala wa Stashahada ya Nishati Jadidifu (Ordinary Diploma in Renewable Energy -NTA Level 4&6) na kuandaa mtaala mpya wa Shahada ya Kwanza ya Uhandisi Tiba (Bachelor of Engineering in Biomedical Engineering -NTA Level 7&8).

Mitaala hiyo miwili imewasilishwa leo mbele ya wadau ili iweze kupitiwa na kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha mitaala hiyo kwa hatua zaidi.

Akifungua mkutano  wa wadau hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam,  Profesa Christopher Mgonja amesema DIT inapitia mitaala yake pamoja na kuanzisha mitaala mipya kwa lengo la kuhakikisha Taasisi inazalisha vijana ambao wanakwenda sambamba na teknolojia mpya.

"Teknolojia inabadilika haraka sana tusipobadilika tutakua nyuma katika teknolojia ya mapinduzi ya nne ya viwanda (4IR), DIT pia tuna dhana yetu iitwayo 'Teaching Factory, ambayo inatuongoza kufanya mafunzo kwa vitendo zaidi ili vijana wanaotoka hapa wasiwe wageni na teknolojia, " amesema Profesa Mgonja.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uhandisi Umeme DIT, Dkt. Godfrey Moshi amesema DIT inajitahidi kuzalisha wataalamu wa kufanya vitu vikubwa na si kuishia kufanya ukarabati wa vifaa badala yake waweze kubuni na kutengeneza kifaa kuendana na teknolojia.

"Tunataka wataalam ambao wamepata mafunzo kwa viwango vya teknolojia ya sasa ndio maana tumehusisha wadau mbalimbali katika sekta hizi ili tupate maoni ya kuboresha mitaala yetu, tupike wataalam ambao wanaweza kujiajiri na sio kusubiri kuajiriwa tu," amesema Dkt.  Moshi.

Amesema katika kozi ya Nishati Jadidifu,  mtaala wake ni wa zaidi ya miaka sita hivyo ni vema kuboreshwa kuingiza mambo mapya ya Teknolojia ya sasa na kwa kozi ya Uhandisi Tiba ni kuendana na uhitaji wa wataalamu hao katika ulimwengu wa sasa.

No comments:

Post a Comment

Pages