Na Dotto Mwaibale, Singida
DIWANI wa Kata ya Mwaru katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Iddi
Athumani Makangale ambaye ni muumini wa dini ya Kiislam ameongoza harambee ya
ununuzi wa vyombo vya muziki vya Kanisa la Waadiventista Wasabato la Kijiji cha
Kaugeri ambapo zaidi ya Sh. Milioni 1.7 zilipatikana.
Akizungumza katika changizo hilo Makangale alisema amejisikia furaha ya
kualikwa kuongoza harambee hiyo hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni Muislam jambo
ambalo limezidi kuongeza mshikamano baina ya Waislam na Wakristo.
" Tukio ili limenipa furaha sana n.a. linaonesha ni jinsi gani waumini
wa hizi dini mbili wanavyoshirikiana katika shughuli zao" alisema
Makangale.
Alisema katika harambee hiyo iliyoonesha mafanikio makubwa jumla ya Sh.
1,785,000 zilipatikana huku ahadi zikiwa ni Sh.470,000.
Diwani Makangale alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi wa dini hizo na
waumini wao kuendelea kudumisha ushiriano huo katika shughuli mbalimbali jambo
litakalosaidia kuharakisha maendeleo katika kata hiyo.
Akizungumza baada ya harambee hiyo Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Geofrey Mgonja alisema wamefarijika sana kwa harambee hiyo
iliyoongozwa na diwani huyo na kueleza ni jambo la kuigwa kwa waumini wote wa
dini hizo.
Alisema tukio la namna hiyo liliwahi kufanywa na Aliyekuwa Rais wa Tano wa
Tanzania Hayati John Pombe Magufuli pale alipoongoza harambee ya ujenzi wa
Msikiti wa Chamwino mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment