Huyu ni mmoja wa watoto wanaopitia Ukatili dhidi ya watoto.
Na Abby Nkungu, Singida
WILAYA ya Ikungi mkoani Singida inakusudia kutumia zaidi ya shilingi
milioni 110 kwa ajili ya utekekezaji wa
shughuli za mradi wa ujenzi wa kituo maalum cha kupinga vitendo mbalimbali vya
ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha wa 2023/24.
Mkuu wa Wilaya hiyo Jerry Muro alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa
Programu Jumuishi ya Taifa kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto
(PJT - MMMAM) inayoendelea hadi 2026.
Alisema kuwa lengo la hatua hiyo ni kudhibiti vitendo vya ukatili wa
kijinsia ambapo takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka
jana hadi Juni mwaka huu, jumla ya watoto 36 wenye umri wa chini ya miaka
minane (0 - 8), wamefanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia.
DC Muro alifafanua kuwa watoto hao wamefanyiwa ukatili wa kingono, kimwili,
kihisia au utekelezaji hivyo kuwasababishia madhara ya kisaikolojia, magonjwa,
ulemavu, kupoteza ndoto zao na haki ya elimu na kuleta ongezeko la watoto waishio
mazingira magumu na hatarishi.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, kesi 9 zipo mahakamani, moja ilifungwa
kituo cha polisi, nyingine iko rufaa Ustawi wa Jamii na zilizobaki watuhumiwa
hawakuweza kupatikana.
Alisema kuwa pamoja na shughuli hiyo kuwemo kwenye utekelezaji wa Programu
Jumuishi ya Taifa, mradi huo mkubwa wa aina yake umetokana na maagizo ya Rais
Samia Suluhu Hassan yanayoelekeza kila wilaya kukomesha matukio na vitendo vya
ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake.
"Mradi huu unafadhiliwa na
Shirika lisilo la kiserikali la KIWOHEDE. Mimi na Mkurugenzi Mtendaji wa
shirika hilo, Mama Justa Mwaituka tumekamilisha mazungumzo na kwa pamoja
tumekubaliana ujenzi wa jengo litakaloitwa MKONO SHUFAA na miundombinu muhimu,
uanze mara moja. Jengo hilo litajengwa katika hospitali ya Wilaya yetu"
alieleza DC Muro.
Alisema kuwa pamoja na ujenzi wa
kituo hicho, pia
wanaendelea kutoa elimu kwenye Jamii na shuleni juu ya namna ya kupinga
ukatili wa kijinsia, kuanzisha kamati za
ulinzi wa mwanamke na mtoto kwa kushirikisha jamii na wadau mbalimbali na
kuendeleza utoaji wa elimu ya Malezi na Makuzi kwa wazazi na Jamii kwa
kushirikisha Jeshi la Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KIWOHEDE, Justa Mwaituka alieleza
kuvutiwa na jinsi ambavyo wilaya hiyo inapambana katika kukomesha vitendo vya
ukatili wa kijinsia katika jamii na kuahidi kuendelea kutoa misaada mbalimbali
ya hali na mali ili kutokomeza vitendo hivyo.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wanasema pamoja na hatua hizo bado kuna haja ya
kutoa elimu zaidi kwa jamii juu ya
umuhimu wa kuzuia na kupinga vitendo vya
ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.
“Jamii yetu bado haina elimu ya kutosha. Unakuta mtu mtoto wake amefanyiwa
ukatili wa kingono kwa kulawitiwa au kubakwa lakini wanamaliza suala hilo
kifamilia. Hii haisaidii kukomessha vitendo hivyo” alieleza Patrick Mdachi
Ofisa Maendeleo ya Jamii mstaafu na kuungwa
mkono na Rehema Daniel aliyetaka viongozi wa Mitaa na Vijiji kuacha
kumaliza masuala hayo ngazi za chini bali wayafikishe kwenye vyombo vya sheria.
Walisema kuwa iwapo hatua za kisheria zitachukuliwa kikamilifu dhidi ya
wahusika wa vitendo vya ukatili kijinsia
kwa watoto, itasadia kutoa funzo na
kuogofya watu wengine wenye nia ovu katika jamii yote.
Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya Wanawake na Watoto katika Hospitali
ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk. Suleiman Muttani anasema kuwa ukatili wa
kijinsia kwa watoto umekuwa na madhara
makubwa kwa kundi hilo na kuleta athari
za kiafya na kisaikosojia kwa muda mrefu na mfupi.
Dk. Muttani ameshauri kuwepo mikakati madhubuti kwa ajili ya kudhibiti
vitendo hivyo katika jamii kwa kuwa baadhi yake vina athari kubwa kwa afya ya
mtoto hata baada ya mtoto huyo kuwa mtu mzima. |
No comments:
Post a Comment