HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 30, 2022

NMB yafungua Tawi Maalum Maonyesho ya SabaSaba

 

Meneja wa Benki NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (wa pili kushoto), akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu ushiriki wa benki hiyo kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, yanayoendelea katika Viwanja vya JK Nyerere Barabara ya Kilwa. Kushoto ni Meneja wa NMB Tawi la Temeke SabaSaba, Kidawa Masoud. (PICHA NA FRANCIS DANDE).


 

KATIKA kukidhi mahitaji na suluhuhishi za kifedha kwa watembeleaji na kampuni shiriki za Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Benki ya NMB imefungua Tawi Maalum liitwalo NMB Sabasaba.


Ufunguzi wa tawi hilo umefanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba mtaa wa Mabalozi ukilenga kuitikia maombi ya washiriki wengi wa maonyesho hayo miaka iliyopita, ambako mwaka huu wameweka tawi hilo na kusambaza Mawakala zaidi ya 50 viwanjani hapo.  

Tawi hilo, ambalo linakwenda kutoa huduma sawa na matawi mengine zaidi ya 226 yaliyotapakaa kote nchini, pamoja na mambo mengine linalenga kuthibitisha kwa vitendo kaulimbiu ya benki hiyo ya; Kushamirisha Mazingira Rafiki ya Biashara na Uwekezaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, NMB Sabasaba iliyopo mtaa wa Mabalozi linaenda kukata kiu ya miaka kadhaa ya huduma za kifedha, hasa ikizingatiwa idadi ya kampuni shiriki na watembeleaji mwaka huu inatarajia kuongezeka.

“Tumejipanga vya kutosha kutoa huduma zote za kibenki hapa, ambapo maonesho haya mwaka huu yanatarajiwa kutembelewa na watu zaidi ya 600,000, huku kukiwa na mabanda zaidi ya 3,000 ya kampuni na taasisi za kitaifa na kimataifa.

“Tutakuwa na wafanyakazi zaidi ya 35, ambao watahudumu katika masuala mbalimbali, ikiwemo dirisha la malipo kwa njia ya ‘control number,’ kwenda kwenye taasisi na mamlaka za Serikali kama RITA, NIDA, TRA na nyinginezo nyingi, ikiwemo ubadilishaji wa fedha za kigeni kwa wageni,” alisema Donatus.

Aliongeza kuwa, NMB itashirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa ajili ya kutoa elimu na ushauri wa kifedha kwa washiriki na wawekezaji, hasa wa kigeni watakaoshiriki maonesho hayo, ili kuwawezesha kuyajua mazingira ya ndani kibiashara na kiuwekezaji.

Kupitia maonesho hayo yaliyofunguliwa Juni 28, NMB inayatumia kunadi huduma mbalimbali zilizo sokoni kwa sasa, na kwa mwaka huu wanaingia katika Sabasaba na Huduma ya Teleza Kidigitali, - mwamvuli unaojumuisha MshikoFasta, NMB Lipa Namba na NMB Pesa Wakala.   

Naye Meneja wa NMB Tawi la Temeke, Kidawa Masoud, ambaye sasa atasimamia Tawi la Sabasaba hadi mwisho wa maonesho hayo, alisema ujio wa tawi hilo ni majibu kivitendo kwa wateja waliokuwa wakihangaika kupata huduma za NMB viwanjani hapo, na kuwataka kutembelea banda lao kuhudumiwa.


No comments:

Post a Comment

Pages