Na Irene Mark
TIMU ya soka ya TASAF imeichakaza timu ya soka ya Umoja wa Mafundi Mkoa wa Dar es Salaam kwa bao nne kwa tatu wakati wa mechi ya kirafiki iliyofanyika jijini Dar es Salaam jioni ya leo Juni 25,2022.
Mchezo huo wa kirafiki uliosheheni ushabiki na mbwembwe, ulihudhuriwa na mamia ya wakazi wa jiji hilo kwenye viwanja vya shule ya Kenton Sinza.
Mechi hiyo ilianza saa 11 jioni huku wachezaji wa timu zote wakiwa na ari ya ushindi chini ya mwamuzi Mussa Saidi.
Magoli ya mawili ya TASAF yalifungwa na James Luhanjo katika kipindi cha kwanza huku magoli mawili ya Umoja wa Mafundi Mkoa wa Dar es Salaam yakifungwa na Abdul Kiduku na Emmanuel Joseph na kufanya kipindi cha kwanza kwenda mapunziko kwa mizania sawa.
Hasira za timu ya TASAF ziliamka kipindi cha pili baada ya James Luhanjo kuongeza bao la tatu lililowaamsha wachezaji wa timu ya Umoja wa Mafundi Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha mpaka dakika ya 79 timu zote kuwa na matokeo sare.
Hata hivyo matokeo hayo hayakudumu baada ya Frank Lyimo kutoka timu ya TASAF kupachika bao la nne lililodumu hadi mwisho wa mpambano huo na kupeleka ushindi kwa timu yake.
Akizungumzia kandanda hilo, mwamuzi wa kati, Saidi amesema ni mpambano uliokuwa na kasi kwa wachezaji wa pande zote mbili.
Mwalimu wa timu ya TASAF, Ramadhan Salum amesema matokeo hayo yamemfariji na kuona namna timu yake inavyozidi kupata muunganiko.
“Tukipata muda wa kukaa na kufanya mazoezi pamoja walau mara siku saba kabla ya mechi kutaongeza ubora wa timu yangu na kuleta matokeo mazuri zaidi ya haya,” amesema mwalimu Salum.
Kwa upande wake mwalimu wa timu ya Umoja wa Mafundi Mkoa wa Dar es Salaam, Deo George amesema matokeo hayo yamemsaidia kuona maeneo ya kufanya maboresho kwa ajili ya matokeo mazuri wakati ujao.
No comments:
Post a Comment