NA TATU MOHAMED
MKURUGENZI
Mtendaji wa BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Dk. Anselm
Moshi amesema kuwa zaidi ya wakulima 6000 nchini wameingia katika mfumo
wa kulima kilimo cha mkataba.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana katika maonesho ya 46
ya kimataifa ya biashara, Dk. Moshi alisema kilimo hicho cha mkataba
kitamsaidia mkulima kurejesha gharama zake alizotumia wakati wa kuandaa
shamba na kuuza mazao yake yote aliyoyavuna.
Amesema
bodi hiyo inaendesha kilimo hicho cha mkataba na tayari wameshaanza
katika zao la ngano maeneo ya Kaskazini huko Kilimanjaro eneo la Siha,
mkoani Arusha eneo la Monduli, Karatu, Semanjiro na Manyara eneo la
Hanang.
“Maeneo hayo yote
tumeingia mkataba na wakulima wa kilimo cha ngano kuzalisha zao hilo,
lakini pia tunafanya kilimo cha mkataba kwenye maharage ya soya na
tumeshaanza kwenye mkoa wa Songea,” alisema MOshi
Amesema
wameshaanza kilimo mkataba kwenye zao la alzerti katika mikoa ya
Singida, Dodoma na Simiyu huku mpango wao ni kuhakikisha kwenye mazao
yote wakulima wanalima kwa kilimo cha mkataba ili kuwa na uhakikika wa
mazao yao kununuliwa bila kupata hasara.
"Kilimo
hicho cha mkataba huo unasainiwa na taasisi tano ambazo ni mkulima
mwenyewe ambaye ndiyo mzalishaji, benki watoaji wa fedha, wasambazaji
pembejeo pamoja na mtu wa bima ambaye ndiyo mnunuzi," amesema Moshi.
Amesema
ili kuhakikisha mkulima anakuwa na soko la uhakika kwa ajili ya mazao
yao, bodi hiyo ya CPB inajenga viwanda kwa wingi katika kila eneo la
nchi ambavyo pia vitatoa ajira kwa vijana, kuongeza thamani ya mazao
yanayozaliishwa ili yaweze kuuzwa katika soko la kimataifa kwa faida
kubwa zaidi kisha kuiletea nchi fedha za kigeni.
Ameongeza
kuwa bodi hiyo lengo lake ni kuhakikisha mkulima mdogo mdogo wa
Tanzania anapata bei shindani katika mazao yake anayoyazalisha kwa
kujenga uwezo mkubwa wa kuweza kununua mazao ya mkulima kwa bei
shindani.
“Tunatekeleza
hayo kwa kufanya uchambuzi wa kufahamu na kujua mkulima anatumia kiasi
gani shambani na kwamba tukinunua kwa bei gani mazao yake anaweza
kurejesha gharama alizozitumia na kupata faida,” amesema Moshi.
“Kwa
sababu tunanunua sisi kwa wingi inawafanya wafanyabiashara wengine
kununua kwa bei hiyo hiyo ya kwetu, hivyo kufanya mkulima kurudisha
gharama zake, kupata faida na kuhamasika kwenda kulima tena huku nchi
kuwa na usalama wa chakula,” amesema Moshi.
Aidha
Dk. Moshi amesema serikali imetoa maelekezo kwa bodi hiyo kuhakikisha
kuwa ngano inazalishwa hapa nchini hadi kufikia tani milioni moja na
zaidi ifikapo 2025.
Amesema
katika kutekeleza mkakati huo mwaka 2021 waliagiza Mbegu za tani 210
nchini Zambia na kuzigawa kwa wakulima kwa mkopo katika kanda ya
Kaskazini na matokeo yalikuwa mazuri.
Amesisitiza
kuwa Mwaka huu wamejipanga kwasababu kuna mbegu zimezalishwa ndani ya
nchi na serikali imeweka jitihada kupitia taasisi za Taasisi ya Utafiti
wa Kilimo Tanzania (TARI) na Kampuni ya kuzalisha mbegu ya ASA ili
kuweza kuzalisha mbegu nchini.
No comments:
Post a Comment