HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 11, 2022

SMZ yatoa bei elekezi ya Mchanga

Na Talib Uss, Zanzibar


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema itamchukulia hatua mwananchi atakayefanya biashara ya mchanga bila kufuata utaratibu, Wizara ya Maji, Nishati na Madini (WMNM) imeshatoa maelekezo katika ununuzi wa  maliasili hiyo huku ikitoa bei elekezi.
 
Akizungumza  na waandishi wa habari Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaaban Ali Othman wakati akitoa taarifa  ya ufunguzi wa shimo jipya la mchanga  katika ukumbi wa jengo la ZURA alisema uuzaji wa maliasili zisizorejesheka unafanywa na  Serikali na sio mwananchi. Hivyo hatuka kali za sheria zitachukuliwa kwa atayefanya biashara ya mchanga Zanzibar.
 
Mhe. Othman alisema SMZ imeweka utaratibu maalum wa kufungua na kufunga mashimo ya mchanga na wananchi wanatakiwa kununua kupitia tovuti https://madinismz.go.tz/ huo ndio utaratibu ambao umewekwa kwa wanaanchi wenye mahitaji ya mchanga kwaajili ya ujenzi na sio kupitia kwa mtu binafsi.
 
Alisema Wizara ya Maji, Nishati na Madini (WMNM) siku ya Julai 12, 2022 inafungua shimbo jipya la mchanga eneo la Bwimbuni Misufini la familia ya Bw. Juma Mwinyi liliyopo Wilaya Kaskazini ‘B” Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
 
“WMNM inafungua shimbo jipya la mchanga eneo la Bwimbuni Misufini la familia ya Juma Mwinyi na inafunga shimo la ndugu Asha Ibrahim liliopo Donge Mchangani ambalo lilikuwa likitumika kwa matumizi ya kawaida ya wananchi’ Alisema Naibu Waziri huyo.
 
Alifahamisha bei elekezi kwa tani moja (1) ya mchanga ni shilingi elfu kumi (10,000) ambayo elfu saba 7,000 zitalipwa kupitia akaunti ya Wizara na elfu tatu (3,000) italipwa kwa akaunti ya mwenye shamba. Hivyo wananchi wasinunue maliasili hiyo kwa watu ambao wanafanya ulanguzi.
 
Aidha akijibu swali la mwandishi aliyeta kujua sifa ya kufungua shimo la mchanga, Mhe Othman alisema sifa ziko nyingi lakini kati ya sifa hizo moja wapo shamba linatakiwa liwe halali kwa mmliki na baada ya hapo wataalum wanafanye tathmini lisiwe karibu na bahari, makaburi wala katika eneo la hifadhi ya misitu.

No comments:

Post a Comment

Pages