Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani hapa imebaini
mianya mbalimbali ya upotevu wa mapato katika baadhi ya halmashauri sanjari na
matumizi ya fedha mbichi kwa visingizio vya changamoto za kimtandao.
Aidha, Taasisi hiyo pamoja na mambo mengine, imefanya chambuzi katika sekta
ya madini ya ujenzi, uvuvi na mapato yatokanayo na makusanyo ya POS na kubaini
kasoro kubwa za mapato hayo kukatiwa stakabadhi mara mbili sambamba na
ucheleweshwaji wa kupelekwa benki.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 10, 2022 na Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Mzalendo Widege wakati
akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ya namna walivyotekeleza majukumu ya
uzuiaji wa vitendo vya rushwa, uchunguzi na elimu kwa umma, kwa kipindi cha
Aprili hadi Juni 2022.
"Kwenye upande wa makusanyo kuna tatizo la baadhi ya watendaji kutumia
fedha mbichi kwa visingizio vya matatizo ya mtandao au umbali wa ofisi za
halmashauri," alisema.
Widege alisema katika kipindi hicho taasisi imechukua hatua kadhaa katika
kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuendesha warsha zilizolenga kuziba
mianya ya rushwa na upotevu wa mapato hususani kwenye maeneo ya sekta ya madini
na mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji.
Pia kwa mujibu Takukuru, katika kipindi hicho wamepokea takribani
malalamiko 70 ya taarifa za rushwa na zisizo za rushwa kwenye maeneo ya ardhi,
serikali za mitaa, mahakama, elimu, polisi, afya na sekta binafsi na uchunguzi
unaendelea.
" Shabaha iliyopo katika robot ya Julai hadi Septemba mwaka huu no kufanya ukaguzi wa miradi, chambuzi za mifumo, warsha na wadau kujadili matokeo ya chambuzi za mifumo ili kuweka maazimio ya namna bora ya juziba mianya ya ufujaji iliyobainika," alisema Widege.
No comments:
Post a Comment