HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 30, 2022

Mtanzania atwaa taji la Miss kiziwi duniani


TANZANIA imeandika historia kwa kunyakua taji la mrembo wa Dunia kwa watu wenye uziwi, ambapo Hadija Kanyama (24) ameibuka mshindi huku Rajan Ally akinyakua nafasi ya pili kwa upande wa wanaume.


Hadija na Rajan, walinyakua mataji hayo juzi wakati wa kinyang’anyiro hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam na kushirikisha washiriki 107, huku Tanzania ambayo ilikuwa mwenyeji ikiwakilishwa na vijana sita.


Akizungumza baada ya kunyakua taji hilo, Hadija alisema ataendelea kuinua vipaji vya watu wengine wenye uziwi waweze kutimiza ndoto zao.


“Kama mimi nilivyojitokeza kushiriki mashindano haya nimeonesha kipaji change, hivyo nataka kujenga jamii jumuishi kwa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika matukio kama haya bila kujali ulemavu walionao,” alisema Hadija. 


Mgeni rasmi katika mashindano hayo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, aliwapongeza washindi na kuwasihi wazazi wenye watoto wenye ulemavu wawaunganishe na fursa mbalimbali kama mashindano hayo ili waweze kuonesha vipaji vyao.


“Kitendo cha kushiriki tu mashindano ni fahari tosha, Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaendelea kupewa fursa na kuaminiwa, sisi sote ni sawa mbele za Mungu, tusibaguane, tupendane,” alisema Dk. Gwajima. 


Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, alisema wataendelea kuibua vipaji vya watu wenye ulemavu na kuviendeleza ili viweze kubadili maisha yao. 


“Tutaendelea kufanya mazuri yale ambayo rais wetu anatamani yatokee kwa Watanzania, tunaamini matukio makubwa ya namna hii hayatakuwa ya kwanza, yataendelea kutokea katika nchi yetu,” alisema Mchengerwa. 


Rais wa Dunia wa Viziwi, Bonita Annleek, alisema watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa kiutendaji kama walivyo wengine na kuiasa jamii kuacha kuwanyanyapaa. 


Washindi hao na washiriki wengine kutoka nchi mbalimbali leo wanatarajia kufanya ziara ya kitalii katika Hifadhi ya Ngorongoro.  


Nchi nyingine zilizoshiriki shindano hilo ni; Australia, Botswana, India, Kenya, Uganda, Korea, Marekani, Msumbiji, Rwanda, Senegal, Sudan Kusini, Ubelgiji, Tunisia, Uingereza, Ujerumani, Vietnam na Zimbabwe. 


Mashindano hayo, yalianzishwa mwaka 2010 ambapo Tanzania ilianza kushiriki mwaka 2021 katika ngazi ya taifa kisha Afrika,  ambapo pia ilipewa nafasi ya kuwa mwenyeji. Mashindano yajayo yanatarajiwa kufanyika nchini Korea.

No comments:

Post a Comment

Pages