HABARI MSETO (HEADER)


November 18, 2022

  Milioni 300 kujenga Kituo cha Afya Vunta

Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango, akitoa machozi ya furaha baada ya kukabidhiwa Sh. Mil. 300  kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kata ya Vunta  na Naibu Waziri TAMISEMI. Dk.Festo Dugange.
 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk.Festo Dugange, akisikiliza jambo  wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo kata ya Vunta wilayani Same mkoani Kilimanjaro
 

Na Mwandishi Wetu, Same

 

SERIKALI imetoa Sh.milioni 300, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya  cha kata ya Vunta wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk.Festo Dugange wakati wa ziara aliyofanya katika Jimbo la Same Mashariki kukagua miradi ya maendeleo.

Alisema Kituo cha Afya Vunta kilichopo kimechakaa, hivyo ni imani yake fedha hizo ambazo zimetolewa na Serikali zitatumika vizuri kujenga upya, ili wananchi waweze kupata huduma bora.

“Majengo yaliyopo yamechaa sana, tumesikia kilio chenu kupitia Mbunge wenu Anne Kilango, Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu Sh.milioni 300 zitolewe kwa ajili ya Vunta naamini mtapata huduma bora kikikamilika,” alisema.

Dk Dugange alitoa maelekezo kwa viongozi wanaohusika kuhakikisha ujenzi huo unaanza mara moja, huku akisisitiza ujenzi huo uzingatie uwepo wa majengo ya upasuaji na chumba cha kuifadhia maiti, ili wananchi wasipate tabu kutembea zaidi ya kilometers 25 kufata huduma ya afya.

Naibu Waziri Dugande alimwagia sifa Mbunge Kilango kwa kuchapa kazi na kuwapigania wapiga kura wakeakiwa bungeni, ili waweze kupata huduma za kijamii bora na nzuri.

Alisema ameridhishwa na miradi  ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Mihamba, zahanati inayogharimu Sh.milioni 500 na  barabara ambazo zitapunguza adha ya usafiri katika  vijiji vya Same Mashariki.

Naye Mbunge Kilango alisema anatoa shukran kwa Rais Samia kwa kuwapatia fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo  cha Afya Vunta ambacho amekuwa akikiombea fedha bungeni mara kwa mara.

Kilango alisema lengo lake ni kuona wananchi wake hawapati tabu kwenye mahitaji muhimu kama afya, elimu, maji na barabara , ili waweze kupitisha mazao yao kwa wepesi  zaidi na kuwapatia wananchi miradi tofauti wajikwamue kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Pages